• HABARI MPYA

    Sunday, February 12, 2017

    KILA LA HERI YANGA COMORO LEO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MABINGWA wa Tanzania, Yanga SC leo wanaanza safari ya kuwania taji la Afrika watakapomenyana na wenyeji, Ngaya Club de Mde mjini Moroni, Comoro.
    Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina anaamini Watanzania wengi wanawachukulia wapinzani wa Comoro kama timu rahisi, lakini kwake anawapa uzito sawa na kigogo chochote cha Afrika.
    “Ukishaingia kwenye mashindano kama haya, hakuna timu rahisi. Unatakiwa kujiandaa vizuri na kucheza kwa makini ili ushinde na kusonga mbele,”alisema Lwandamina kabla ya kuondoka kwenda Moroni juzi.  
    Lwandamina aliondoka jana Alfajiri na kikosi cha wachezaji 20, tayari kabisa kwa mchezo huo wa leo wa kwanza wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika. 
    Katika mchezo wa leo, Yanga itamkosa mshambuliaji wake tegemeo, Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma ambaye amebaki Dar es Salaam kutokana na kuwa majeruhi baada ya kuumia katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Stand United Ijumaa iliyopita.
    Pamoja na Ngoma, wengine watakaokosekana leo ni kipa Benno Kakolanya, mabeki Mtogo Vincent Bossou, Pato Ngonyani, Andrew Vincent ‘Dante’ na washambuliaji Malimi Busungu, Matheo Anthony.
    Lwandamina amewaacha Kakolanya, Matheo, Bossou na Ngonyani kwa sababu hawamo katika programu zake za mchezo huo, wakati Dante anatumia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mechi ya mwisho ya Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe mjini Lubumbashi, DRC Agosti, mwaka jana – na Busungu mgonjwa.
    Wachezaji waliopo Comoro na Yanga ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’. Mabeki ni Juma Abdul, Hassan Kessy, Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondani, 
    Viungo ni Deus Kaseke, Haruna Niyonzima, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Saidi Juma ‘Makapu’, Juma Mahadhi, Yusuph Mhilu, Obrey Chirwa, Justine Zulu  na Emmanuel Martin wakati mshambuliaji ni Amissi Tambwe pekee.
    Benchi la ufundi linaongozwa na Kocha Mkuu; George Lwandamina, Kocha wa Viungo, Noel Mwandila wote Wazambia, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa Makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Daktari Edward Bavu, Watunza Vifaa, Mohamed Omary Mwaliga na mchua misuli Jacob Sospeter Onyango.
    Msafara huo utakuwa chini ya mwakilishi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mussa Mohammed Kisoki na Paul Malume wa Yanga. Mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 18 na mshindi atakutana na Zanaco ya Zambia katika Raundi ya Kwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI YANGA COMORO LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top