• HABARI MPYA

    Thursday, February 09, 2017

    KANGWA AREJEA KUONGEZA NGUVU AZAM FC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAKATI winga wa kushoto wa Azam FC, Bruce Kangwa, akianza rasmi kujifua jana jioni baada ya kuwasili nchini juzi, nahodha John Bocco, aliyekuwa majeruhi naye ameanza rasmi mazoezi mepesi kufuatia kuanza kujisikia nafuu.
    Kangwa alikosekena kwenye kikosi cha Azam FC tokea mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana baada ya kuelekea nchini Gabon kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) akiliwakilisha Taifa lake la Zimbabwe, ambalo liliishia hatua ya makundi.
    Beki huyo ameonekana kurejea na kasi yake kama aliyoondoka nayo, hali ambayo ilimpa urahisi kwenye maelekezo aliyokuwa akipewa na Kocha Mkuu, Aristica Cioaba.
    Bocco anasumbuliwa na misuli ya paja baada ya kuichana wakati Azam FC ikiifunga Simba bao 1-0 wiki moja iliyopita, huku yeye akiwa mfungaji wa bao hilo lililowazamisha wekundu hao.
    Mbali na Bocco, wachezaji wengine ambao ni wagonjwa ni kiungo Stephan Kingue, anayesumbuliwa na tatizo kama la Bocco na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye ameshindwa kuendelea na programu ya mazoezi leo baada ya kutonesha tatizo linalomkabili kwenye vidole vya mguu wake wa kulia.
    Kwa mujibu wa taarifa ya Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, Bocco anaendelea vema na ataendelea na programu hiyo ya mazoezi mepesi hadi mwishoni mwa wiki hii. “Tunamshukuru Mungu Bocco anaendelea vema, anatarajia kuendelea na programu ya mazoezi mepesi hadi mwishoni wa wiki hii, Jumatatu ataungana na Stephan (Kingue) kuanza mazoezi na wenzao na hapo ndipo tutaangalia maendeleo yao kabla ya kuanza kutumika kwa mechi za kuanzia wiki ijayo,” alisema.
    Kikosi cha Azam FC kimeingia kambini tokea Jumanne iliyopita, kikifanya mazoezi makali kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ruvu Shooting, utakaofanyika Uwanja wa Mabatini, Pwani Jumamosi ijayo saa 10.00 jioni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KANGWA AREJEA KUONGEZA NGUVU AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top