• HABARI MPYA

    Sunday, February 19, 2017

    JUMAMOSI NI SIMBA NA YANGA TENA, TFF INATUAMBIAJE KUHUSU MAREFA?

    OKTOBA 1, mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam uligeuka kilinge cha mapambano baina ya Polisi na mashabiki wa Simba, wakati wa mchezo dhidi ya mahasimu wao, Yanga.
    Vurugu zilizuka dakika ya 26 jana katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya mshambuliaji wa Yanga, Mrundi Amissi Joselyn Tambwe kuifungia bao la kuongoza timu yake.
    Tatizo halikuwa kufunga, bali lilikuwa bao la utata, kwani Tambwe alilalizimika kutumia mkono kuiweka sawa katika himaya yake pasi ya Mkongo, Mbuyu Twite kabla ya kumchambua kipa Muivory Coast, Vincent Angban.
    Wachezaji wa Simba walimfuta refa, Martin Saanya kulalamikia bao hilo na wakati huo huo mashabiki wao wakaanza kung’oa viti na kuvirusha uwanjani.
    Ikabidi Polisi waanze kupambana na mashabiki hao kwa kuwafyatulia moshi wa gesi za machozi ili kuwatuliza – jambo ambalo lilifanikiwa na mchezo ukaendelea.
    Lakini Saanya akajikuta katika wakati mgumu zaidi baada ya kumtoa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja, kiungo na Nahodha wa Simba, Jonas Gerald Mkude aliyekuwa mstari wa mbele katika kumghasi.
    Amani ilichafuka kwa muda fulani Uwanja wa Taifa, katika mchezo ambao ulihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Mchemba na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe. 
    Baadaye refa Saanya na msaidizi wake namba moja, waliondolewa katika orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu na Mkude alifutiwa kadi nyekundu. 
    Kwa ujumla tukio la Oktoba 1, lilikumbushia tukio la Machi 31, mwaka 2002 katika fainali ya Kombe la Tusker, Simba ikishinda 4-1.
    Siku hiyo refa Abdulkadir Omar ‘Msomali’ aliivuruga mechi na kuhatarisha amani uwanjani pia kwa madudu yake.
    Kwa nini? Katika mechi hiyo ya fainali iliyohudhuriwa na rais mstaafu wa awamu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka Suleiman kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. 
    Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. 
    Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, (FAT), sasa TFF kabla ya kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo baadaye.
    Ni marefa wachache sana wamewahi kuziongoza vizuri mechi za Simba na Yanga na zikamalizika bila manung’uniko, akiwemo mwanamama mwenye beji ya FIFA, Donisya Rukyaa wa Kagera anayefuata nyayo za marefa wakongwe kama Nassor Hamdon wa Kigoma.
    Wiki hii Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Zimbabwe, Method Mwanjali, ambaye pia ni beki wa zamani wa mabingwa wa Afrika, Mamelodu Sundowns alisema Simba na Yanga ni kati ya mechi kubwa za wapinzani wa jadi Afrika.
    Unaweza kutilia shaka kiwango cha soka cha timu hizo, lakini si upinzani wao kwa maana ya upinzani na hamasa za kishabiki. Watu wanazimia na wengine kufa, kujiua kwa sababu ya Simba na Yanga.
    Upinzani wao ni sehemu ya burudani na kama iko siku zitakuwa timu imara na kucheza soka ya kuvutia, basi burudani itakuwa mara mbili.
    Hata hivyo kuna mambo mawili au matatu ambayo kwa kiasi fulani yamekuwa yakipunguza ladha ya mechi za watani hao wa jadi.
    Awali tatizo kubwa lilikuwa Uwanja mdogo wa Uhuru, lakini tangu kukamilika kwa Uwanja wa Taifa ambao tumeshuhudia mechi zote zilizochezwa hapo, haijatokea mechi hata moja mashabiki wakajaza viti, mambo yamekuwa mazuri.
    Matatizo mawili yaliyobakia ni viwango vya timu kuboreshwa, ili ifike wakati pamoja na upinzani na kukamiana lakini watazamaji washuhudie soka safi.
    Tatizo la pili ni marefa, kweli ilipofikia na kama kweli lengo ni kuiongezea msisimko zaidi mechi ya watani, waamuzi wa Tanzania wawekwe kando na watumike waamuzi kutoka nje ya nchi, tena ikibidi nje kabisa ya nchi tatu za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.
    Rejea hata mchezo wa Machi 5, mwaka 2011 Uwanja wa Taifa, refa Orden Mbaga aliivuruga mno mechi hiyo, kutokana tu na pengine mchecheto ama kutaka kufanya kile ambacho kinaitwa ‘kubalansi’ mchezo au kukwepa lawama, matokeo yake akafanya madudu.
    Dakika ya 58 Juma Said Nyosso alimkwatua Mzambia Davies Robby Mwape kwenye eneo la hatari akawapa penalti Yanga na kilichofuatia wengi walijua beki huyo wa Simba atatolewa nje kwa kadi nyekundu, badala yake akampa kadi ya njano.
    Ngumu kuamini Mbaga, refa mwenye beji ya Shrikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hajui alipaswa kufanya nini kwa Nyosso, lakini kwa sababu ni refa wa nyumbani na aliongoza wapinzani wa jadi katika mechi ya nyumbani, alihofia kumtoa mchezaji kwa kadi nyekundu angeshushiwa lawama nzito. Marefa hufanyiwa fujo na kupigwa na mashabiki, labda alihofia hali hiyo pia.
    Dakika ya 73 Simba walipata bao safi la kusawazisha lililofungwa kwa kichwa na Mussa Hassan Mgosi, aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Mghana Yaw Berko kufuatia shuti la mpira wa adhabu, lililogonga mwamba wa juu na kudondokea nyavuni kabla ya kuokolewa na mabeki wa Yanga.
    Halikuwa bao lenye shaka yoyote, hakukuwa na kuotea wala dosari yoyote, lakini haieleweki kwa nini Mbaga alilikataa bao hilo awali.
    Ilikuwa offside au mpira haukutinga nyavuni hadi akalikataa kwanza? Haijulikani, lakini alilikubali baada ya wachezaji wa Simba kumuambia aangalie kwenye TV kubwa iliyopo uwanjani marudio ya tukio lile na baada ya hapo akaenda kujadiliana na msaidizi wake, ndipo akalikubali.
    Tujiulize, kusingekuwa na ile TV, Simba wangedhulumiwa bao lao?
    Mbaga alichemsha- lakini si Mbaga tu, marefa wengi wa Tanzania waliwahi kutokota kabla yake na nitakumbushia baadhi ya mechi.   
    Agosti 18, mwaka 2002 Simba na Yanga zikitoka sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu, refa Victor Mwandike aliwaacha mashabiki wa Simba midomo wazi kwa kuwapa Yanga penalti ya utata dakika ya 89 na ushei, ambayo Sekilojo Chambua aliitumia vema kuisawazishia bao timu yake, baada ya Simba kutangulia kufunga kupitia kwa Madaraka Suleiman dakika ya 65.
    Oktoba 24, mwaka 2007, refa Osman Kazi alikataa mabao matatu yaliyofungwa na Yanga, yote akidai kipa Juma Kaseja alisukumwa na wachezaji wa Yanga, lakini kwa yeyote atakayerudia kuangalia DVD ya mchezo ule, hawezi kuona ukweli wa madai ya Kazi.
    Awali ya hapo, Kazi aliwahi kupuliza filimbi ya kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la Tusker mwaka 2005 mjini Mwanza, wakati mchezaji wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ amekwishawatoka mabeki wa Simba na anakwenda na mpira mbele yake amebaki Juma Kaseja tu.
    Refa ni mwamuzi wa mwisho- lakini kwa wana Yanga walijutia mno tukio lile kwenye mchezo ambao mwishowe walifungwa 2-0, kwa mabao ya kipindi cha pili ya Emmanuel Gabriel na Mussa Mgosi.
    Aprili 19, mwaka 2009, Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la kusawazisha kwa mkono na kutengeneza sare ya 2-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Refa makini asingeweza kukubali bao lile, hivyo kwa haya yote lazima tukubali marefa wa Tanzania hawawezi tena kuchezesha mechi za watani wa jadi.
    Sababu nyingine za marefa wetu kuzishindwa mechi hizo ni hiyo ya mapenzi yao kwa moja ya timu hizo, kitu ambacho Misri wamekiepuka na mechi ya Zamalek na Ahly inachezeshwa na marefa kutoka nje ya nchi yao.
    Nakumbuka refa kutoka Uganda, Dennis Bate aliyechezesha fainali ya mwisho ya Kombe la Tusker mwaka 2009 kati ya Simba na Yanga, aliiongoza vizuri mechi hiyo na akadhibiti ujanja wote wa wachezaji kutaka kumdanganya na hatimaye aboronge.
    Kuna wachezaji wanaitwa wazoefu wa mechi za Simba na Yanga na hawa wamekuwa wakiwapoteza sana marefa kwa uzoefu wa kucheza mechi hizo, lakini kama marefa watatoka nje ya Tanzania, tena wa kiwango cha beji za FIFA, uhondo wa mechi za watani utaongezeka maradufu. 
    Baada ya balaa lililoababisha na refa Saanya Oktoba 1, miamba hiyo itakutana Jumamosi ijayo katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu pale pale Taifa. 
    Je, safari hii TFF itampa refa gani mechi ya Februari 25? Hilo ndilo swali.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JUMAMOSI NI SIMBA NA YANGA TENA, TFF INATUAMBIAJE KUHUSU MAREFA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top