• HABARI MPYA

  Monday, February 06, 2017

  AZAM YAIADABISHA NDANDA, KIMOJA TU...YAHAYA HUYO!

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NANI wa kuizuia Azam FC? Ndivyo unavyoweza kuuliza hivyo kutokana na Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati kuendeleza kasi yake, ikiichapa Ndanda bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi usiku wa jana.
  Ushindi huo unafuatiwa na ule mwingine kama huo walioupata wikiendi iliyopita kwa kuifunga Simba, ambapo hivi sasa Azam FC imerejea nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 37 sawa na Kagera Sugar, ikizidiwa pointi 12 na kinara Yanga aliyejikusanyia 49 na Simba 48 katika nafasi ya pili.
  Iliwachukua Azam FC dakika 85 kuweza kupata bao hilo pekee, lililofungwa na Yahaya Mohammed aliyemaliza pasi safi ya juu ya Nahodha Msaidizi aliyekuwa nahodha wa mchezo wa leo, Himid Mao ‘Ninja’.
  Hilo ni bao la pili kwa Yahaya ndani ya ligi tokea asajiliwe kwenye dirisha dogo na la nne baada ya kufunga jingine katika michuano ya Kombe la Mapinduzi wakati Azam FC ikiilaza Yanga mabao 4-0 na jingine akitupia kwenye mchezo wa kirafiki dhidi Ruvu Shooting.
  Azam FC ingeweza kujipatia mabao zaidi, kama ingekuwa makini kipindi cha kwanza kwa nafasi zilizopotezwa na Yahaya dakika ya 21 alipopiga shuti na kupanguliwa na kipa wa Ndanda na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
  Yahaya alikosa nafasi nyingine dakika ya 37 baada ya kuchelewa kupiga mpira, na hata alipopiga kipa wa Ndanda alikuwa tayari ameshafika karibu yake na mpira huo kumbabua kabla ya kuudaka.
  Mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili ya kuingia Samuel Afful, Ramadhan Singano, Mudathir Yahya, yaliongeza uhai kwenye eneo la ushambuliaji la Azam FC hali iliyopelekea kupatikana kwa bao hilo pekee.
  Mshambuliaji wa Azam FC, Shaaban Idd, itabidi ajilaumu mwenyewe dakika ya 51 baada ya kukosa nafasi ya wazi akiwa anatazamana na kipa wa Ndanda kufuatia kupiga shuti lililotoka sentimita chache ya lango la Ndanda.
  Baada ya kucheza kwa kiwango kikubwa kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundo10wns, kiungo chipukizi wa Azam FC, Abdallah Masoud ‘Cabaye’, leo alicheza mechi yake ya kwanza ya ligi baada ya kukalia benchi katika baadhi ya michezo tokea apandishwe kikosi cha wakubwa msimu huu.
  Kabla ya mtanange huo uliokuwa mkali na wa aina yake kuanza, timu zote mbili pamoja na watu wote waliohudhuria uwanjani walisimama kimya kwa dakika moja kama ishara ya kuomboleza kifo cha aliyekuwa kipa wa Kagera Sugar, David Burhan, aliyefariki dunia mwanzoni mwa wiki iliyopita.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Himid Mao (C), Abdallah Masoud/Afful dk 56, Frank Domayo, Yahaya Mohammed, Shaaban Idd/Mudathir dk 80, Joseph Mahundi/Singano dk 68.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM YAIADABISHA NDANDA, KIMOJA TU...YAHAYA HUYO! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top