• HABARI MPYA

    Sunday, February 12, 2017

    ASANTENI LUFUNGA, HAJIB HAYA NI MAJIBU TOSHA KWAO

    BEKI wa kati, Novaty Lufunga amecheza vizuri katika mechi mbili mfululizo za Simba ikishinda mabao 3-0 mara zote katika Ligi Kuu ya Vodadom Tanzania Bara.
    Lufunga alisimama beki ya kati pamoja na Method Mwanjali katika mchezo dhidi ya Maji Maji na akacheza vizuri Simba ikishinda 3-0 Jumamosi ya wiki iliyopita.
    Na wiki moja baadaye tena, jana mchezaji huyo aliyesajiliwa msimu huu kutoka African Sports ya Tanga akasimama na Mwanjali tena Simba ikashinda 3-0 dhidi ya Prisons Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Haya ni mapinduzi makubwa kwake binafsi, Lufunga kwani alikwishaanza kuchungulia mlango wa kutokea baada ya kuanza kukandiwa na wadau wa klabu hiyo juu ya uchezaji wake.
    Ilikuwa inaelezwa ana makosa mengi na anafungisha sana timu na akatuhumiwa hata kutomdhibiti vizuri Amissi Tambwe wa Yanga akafunga bao Oktoba 1, katika sare ya 1-1.
    Kabla ya Simba kwenda kucheza na Maji Maji, ilifungwa 1-0 na Azam FC  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na siku hiyo beki anayeaminika zaidi, Method Mwanjali ndiye aliyefanya kosa lililowazawadia bao wapinzani.
    Binafsi nilijiuliza siku ile uwanjani, kosa lile kama angefanya Lufunga, au Abdi Banda hali ingekuwaje?
    Ikumbukwe Banda naye amekwishaingia kwenye orodha ya wachezaji wa kutiliwa shaka Simba baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Yanga.
    Hiyo ilimgharimu Banda akaanza kuwekwa benchi, kabla ya kuanza kupangwa tena kufuatia Lufunga kuanza kuonekana hafai na Juuko Murshid kuwa na timu yake ya taifa, Uganda.
    Bahati mbaya Banda ameumia na beki mwingine wa kati ni Lufunga, ambaye sasa anacheza na Mwanjali, ambaye jana naye ameumia na kutolewa kwa machela.
    Kama ni maumivu makubwa kiasi kwamba hataweza kucheza mechi ijayo dhidi ya Yanga, haitakuwa ajabu Lufunga na Banda wakachezeshwa pamoja mechi ya watani, iwapo Juuko hatakuwa fiti naye.
    Kuna kitu ninataka kuwakumbusha wana Simba, beki Kevin Yondan alijiunga na Yanga akitoka kwao, Msimbazi na alilazimika kuondoka kwa sababu maneno yalizidi dhidi yake.
    Alikuwa anaonekana msaliti, mara ana makosa mengi na kwa kifupi alikuwa hana amani ya maisha Msimbazi na ilipotokea nafasi ya kwenda Yanga, hakuichezea. Akaitumia vizuri.
    Sasa Yondan amesahau maisha yake ya nyuma ya masimango pale Simba SC na anamalizia soka vizuri Jangwani. Kama asingehamia Yanga, Yondan angekuwa bado yupo Simba leo? Sijui!
    Kuna kitu viongozi wa Simba wanatakiwa kujifunza na zaidi ni hatua za mchezaji kupitia hadi kuwa bora na mzoefu wa aina ya Mwanjali waliyekwenda kumsajili kwa dola za Kimarekani Zimbabwe akiwa tayari amechoka baada ya kutumika kwa muda mrefu Afrika Kusini.
    Na hiyo ni kwa sababu limekuwa tatizo sugu pale Simba namna ya kuishi na wachezaji na ukifuatilia sana hicho ndicho kimechangia hata kuyumba kwa klabu hiyo miaka ya karibuni.
    Wachezaji wengi huondoka Simba SC katika kipindi ambacho ndiyo wanatakiwa kuanza kuisaidia timu.
    Ibrahim Hajib amefunga mfululizo mechi hizi mbili za 3-0 na jana alitoa na pasi ya bao pia, lakini maisha aliyopitia hapa katikati Simba ni magumu. Kwa kifupi alikwishaanza kuonekana hafai.
    Ilikwishaanza kuzungumzwa eti haisaidii timu, lakini alichokifanya katika mechi mbili zilizopita baada ya kupewa nafasi ni majibu tosha. Ndiyo maana mara zote alipofunga hata kutoa pasi ya bao, alikwenda kumsujudia Mungu wake.
    Yapo mambo viongozi wa Simba SC chini ya Rais Evans Aveva na sahiba zake wote akina Mulsey Ruweih, Kassim Dewji na Salim Abdallah ‘Try Again’ wanatakiwa kujifunza na kuanza kubadilika, kwa manufaa ya klabu hiyo.
    Wajifunze kuwavumilia wachezaji, huku wakiwaongoza kama wazazi na zaidi kuwapa majukumu kamili benchi la ufundi juu ya mwenendo mzima wa wachezaji.
    Tazama leo Lufunga anacheza vizuri na kuisaidia timu, kadhalika na Hajib. Je, wale walioanza kuwaona wachezaji hao si kitu wanasemaje sasa?  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ASANTENI LUFUNGA, HAJIB HAYA NI MAJIBU TOSHA KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top