• HABARI MPYA

  Tuesday, January 03, 2017

  YANGA YAKOMALIA POINTI ZA AFRICAN LYON HADI KIELEWEKE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa Yanga umetilia mkazo rufaa yake dhidi ya African Lyon kumchezesha mchezaji wa Mbao FC, Venence Ludovick kuhakikisha inapewa pointi.
  Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedi aliiambia Bin Zubeiry Sports - Online jana kwamba kanuni zipo wazi kwamba timu inapomchezesha mchezaji ambaye si halali inapaswa kupokonywa pointi.
  “Hatushitushwi na propaganda zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba eti Lyon haina makosa kumtumia mchezaji huyo kwa sababu walipewa leseni na TFF, sisi tunatazama kanuni zinasemaje”alisema Deusdedit.
  Aidha, Katibu huyo wa Yanga alisema kwamba wanalifuatilia kwa makini suala hilo ili kuhakikisha haki inatendeka. 
  Yanga imeikatia rufaa African Lyon kwa kumtumia mchezaji Venence Ludovick Desemba 23, mwaka jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliomalizika kwa sare ya 1-1 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa madai ni mali ya Mbao FC ya Mwanza.
  Mbao pia imekata rufaa na kuweka pingamizi Lyon kumtumia mchezaji hiyo. Ludovick aliichezea Mbao mzunguko wa kwanza, kabla ya mzunguko wa pili kuhamia Lyon na akafunga bao katika sare ya 1-1 na Yanga.
  Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema suala la mchezaji huyo linaendelea kufanyiwa kazi na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji. “Tunawahakikishia umma wa wapenda soka nchini kuwa haki itatendeka kwa mujibu wa kanuni zinazoendesha mashindano husika,”ilisema taarifa ya TFF mwishoni mwa wiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAKOMALIA POINTI ZA AFRICAN LYON HADI KIELEWEKE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top