• HABARI MPYA

  Monday, January 02, 2017

  YANGA YAANZA NA MOTO KOMBE LA MAPINDUZI, JAMHURI YAFA 6-0

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  YANGA SC imeanza kwa kishindo michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar baada ya kuichapa mabao 6-0 Jamhuri ya Pemba usiku huu Uwanja wa Amaan.
  Ushindi huo, unaifanya Yanga iongoze Kundi B, kwa pointi zake tatu sawa na Azam iliyoshinda 1-0 dhidi ya Zimamoto katika mchezo wa kwanza jioni ya leo.
  Winga Simon Msuva alifungua biashara nzuri dakika ya 19 akiifungia Yanga bao la  kwanza kwa kumalizia kona maridadi ya Nahodha, kiungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda.
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma akaifungia Yanga mabao mawili mfululizo daakika ya 23 akimalizia krosi ya Mwinyi Hajji Mngwali na dakika ya 37 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa, Omary Said kufuatia shuti la Msuva.
  Donald Ngoma (kushoto) akikimbia kushangilia baada ya kufunga, huku mabeki wa Jamhuri wakiwa wameduwaa

  Msuva tena akawainua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kufunga baola nne dakika ya 40 akitumia makosa ya kiopa kutoka langoni bila mahesabu.
  Baada ya kumaliza kipindi cha kwanza na mtaji wa mabao 4-0, kocha wa Yanga, George Lwandamina akakianza kipindi cha pili kwa mabadiliko, akimpumzisha kiungo Mzambai mwenzake, Justin Zulu na nafasi yake kuchukuliwa na mzalendo, Said Juma ‘Makapu’.
  Kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko akaifungia Yanga bao la tano dakika ya 59 akimalizia krosi ya Juma Abdul, kabla ya kiungo Juma Mahadhi⁠⁠⁠⁠⁠ aliyetokea benchi pia kipindi cha pili kuhitisha tafrija za mabao kwa kufunga la sita dakika ya 85 kwa shuti la karibu.
  Katika mchezo huo, nafasi pekee nzuri ambayo Jamhuri walipoteza ilikuwa ni mapema atu dakika ya 13 baada ya krosi ya Ahmed Ali kuokolewa na beki wa Yanga Andrew Vincent ‘Dante’ na  kuwa  kona  iliyochongwa  na Mohamed  omary  ambayo  haikuza  matunda  baada  ya  beki  huyo kuokoa tena.
  Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondan/Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dk72, Vincent Andrew ‘Dante’, Justin Zulu, Simoni Msuva/Geoffrey Mwashiuya dk77, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma/Juma Mahadhi dk66, Haruna Niyonzima/Deus Kaseke dk66 na Emmanuel Martin.
  Jamhuri: Omary Said, Mohammed Mgau, Mohammed Omary, Mohammed Juma, Yussuf Makame,  Greyson Gerald, Umry Bagaseka, Mbarouk  Suleiman, Mwalimu  Mohammed, Ahmed Ally na  Mussa Mbarouk.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAANZA NA MOTO KOMBE LA MAPINDUZI, JAMHURI YAFA 6-0 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top