• HABARI MPYA

    Sunday, January 15, 2017

    YANGA WALIKURUPUKA KUMLETA LWANDAMINA?

    KUFUATIA matokeo mabaya katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, tayari uvumi umeanza kwamba Yanga wanataka kumfukuza kocha wao Mzambia, George Lwandamina.
    Yanga ilifungwa mabao 4-0 na Azam FC katika mchezo wa mwisho wa Kundi B kabla ya kwenda kufungwa kwa penalti 4-2 na Simba SC kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika Nusu Fainali.
    Siku iliyofuata Yanga ikarejea Dar es Salaam tayari kuendelea na michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia kuhitimisha ushiriki wake Mapinduzi.
    Lakini asubuhi ya kuamkia kutolewa na Simba iliibuka na habari kama za tetesi, eti Lwandamina anafukuzwa. Kwa namna zilivyoibuka, zilikuwa ni habari za kupuuza.
    Lakini kwa siku za karibuni, habari za Yanga zimekuwa zikiibuka katika mtindo wa tetesi na baadaye zinakuwa kweli.
    Kufukuzwa kwa kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm kulianza kama tetesi, baadaye akaja kufukuzwa kweli.
    Ujio wa Landamina mwenyewe ulianza kama tetesi, baadaye akaja kweli na kusaini mikataba.
    Na wakati wa kuibuka kwa tetesi zote, mara zote hizo Yanga ilitoa taarifa za kukanusha. Yanga ilikanusha kumfukuza Pluijm na ikakanusha pia kumleta Lwandamina na sasa imekanusha kutaka kumfukuza Mzambia huyo.
    Pluijm mwenyewe aligundua ni kweli atafukuzwa akaamua kujiuzulu, kabla ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuingilia kati kuhakikisha anarajeshwa.
    Mwigulu ni mpenzi na mwanachama wa Yanga, alimfuata kocha huyo na kumsihi asiondoke na akawafuata viongozi wa timu kuwaomba wamrudishe kazini, akafanikiwa.
    Pluijm sasa amerejea Yanga kama Mkurugenzi wa Ufundi na Lwandamina ni Kocha Mkuu.
    Ujio wa ‘Mkata Umeme’ machachari, kiungo Justin Zulu kutoka Zambia taarifa zake zilianza kama tetesi pia, hatimaye akaja kweli.
    Hatuwezi kuzipuuza hizi taarifa za Yanga kutaka kumfukuza Lwandamina, kwa sababu zinaibuka sambamba na tetesi nyingine za mbadala wake.
    Kuna tetesi pia kocha na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa yupo kwenye mazungumzo na klabu arejee Jangwani.
    Mkwasa amejiuzulu ukocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars baada ya kumaliza mkataba wake na kwa sasa hana kazi, hivyo hakuna ajabu akirejea Yanga.
    Lakini mpango wa kufukuzwa kwa Lwandamina kuna mambo mengi ya kujiuliza kwanza, kubwa anafukuzwa kwa sababu gani na baada ya muda gani?
    Lwandamina amekuja Novemba tu na Yanga ilivutiwa naye baada ya kuifikisha Zesco United Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana ikitolewa na Mamelodi Sundowns walioibuka mabingwa.
    Maana yake Yanga ilitaka kuhamishia kwao mafanikio ya Lwandamina akiwa Zesco United. Na Lwandamina akaja na mtu aliyekuwa anafanya naye kazi Zesco, Noel Mwandila kocha wa mazoezi ya viungo akiamini hapo ndiyo ataisuka vizuri Yanga.
    Lakini siku zao za mwanzo tu kazini, zikaanza kuibuka tetesi kwamba wachezaji wa Yanga hawafurahii mazoezi magumu wanaopewa na wachezaji hao.
    Ikumbukwe mapema wakati wa utambulisho wake akiwa ameongozana na Makamu Mwenyekiti wa klabu, Clement Sanga – Lwandamina aliweka wazi kwamba yeye ni muumini wa mazoezi magumu, akiamini ndiyo yanamjenga mchezaji.
    Na inafahamika wachezaji wa Tanzania hulka yao hawapendi mazoezi magumu, akitokea mwalimu mwenye mazoezi magumu humfanyia hujuma aondoke.
    Makocha wengi wamefukuzwa Tanzania kwa sababu hiyo. Wachezaji hucheza chini ya kiwango makusudi mfululizo, timu inafanya vibaya, kocha anafukuzwa.
    Au wachezaji muhimu hujifanya majeruhi katika mechi kadhaa timu ipoteze, mwalimu aonekane hafai. Vitu kama hivyo. Kuhujumu.
    Kama kweli uongozi wa Yanga unafikiria kumfukuza Mzambia huyo, basi tuamini ulikurupuka hata kumleta Lwandamina.
    Maana ilijua inamleta kocha wa aina gani na akawafundishe wachezaji wa aina gani, hivyo kutaka kuachana naye mapema hivi, kunamaanisha  walikurupuka kumleta.
    Na hii wana Yanga wajue klabu yao ina viongozi wa aina gani – wenye kufanya mambo kwa kukurupuka na kufuata mkumbo, si kwa mipango yao.
    Ndiyo maana huwezi kushangaa wachezaji magalasa wanasajiliwa kwa fedha nyingi kila siku, tu kwa sababu wanaoamua nani asajiliwe, nani aaachwe hawana uchungu kwa sababu hawatoi hata senti moja, fedha anatoa Mwenyekiti, Yussuf Manji, ambaye baadaye anaingiza kwenye deni analoidai klabu. 
    Baada ya kusajiliwa ‘wachezaji hatari’ kutoka Zambia, Obrey Chirwa na Justin Zulu sijui deni limefika Bilion ngapi kwa sasa! 
    Watu wenye kufanya mambo yao kitaalamu hawawezi kuanza kuyajutia ndani ya miezi miwili.
    Hakuna shaka Lwandamina ni kocha mzuri, lakini naamini atafaa kufundisha  Yanga yenye wachezaji wengi vijana wadogo watakaohimili vishindo vya mazoezi magumu.
    Kama kuna timu enzi za ujana wangu nilivutiwa nayo sana ni Yanga mwaka 1996 na 1997 ilikuwa ina wachezaji wengi vijana wadogo na walikuwa wanacheza soka ya kuburudisha kabisa.
    Naizungumzia Yanga Black Star chini ya kocha Mkongo, Tambwe Leya (sasa marehemu) ambayo iifika Robo Fainali na Kombe la Washindi na kutolewa na Blackpool ya Zimbabwe.
    Hawakutumia fedha nyingi Yanga kupata timu ile hatari, bali ni matunda ya uwekezaji kwenye timu ya vijana, kwani wachezaji wengi walipandishwa kutoka timu B.
    Sababu ya wachezaji wa B kupelekwa kikosi cha kwanza ilikuwa ni kufukuzwa kwa karibu wachezaji wote mwaka 1994, baada ya tuhuma za kuhujumu mechi dhidi ya Simba kwa kupewa fedha na aliyekuwa mfadhili wa klabu hiyo (jina tumelihifadhi), ambaye wakati huo alikuwa ana upinzani na uongozi wa klabu hiyo. 
    Baadhi ya wachezaji waliobakishwa kikosini baada ya wengine nyota kama Said Mwamba ‘Kizota’, Salum Kabunda ‘Ninja’ kutupiwa virago ni Kenneth Mkapa, Constantine Kimanda, Sekilojo Chambua, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, wengine wote walitimuliwa kwa tuhuma hizo.
    Baada ya hapo, Yanga iliundwa na wachezaji waliokuwa wakiandaliwa na Tambwe Leya Yanga B aliyoiitaBlack Star, ambao ni pamoja na Godwin Mashoto (sasa marehemu), Mzee Abdallah, Anwar Awadh, Maalim Saleh ‘Romario’, Nonda Shaaban na wengineo, waliosajiliwa kutoka timu mbalimbali kuimarisha kikosi kama Bakari Malima, Reuben Mgaza waliotoka Pan African.
    Haikuchukua muda kikosi cha yosso wa Yanga kikawa tishio hata kikaweza kufika Robo Fainali ya Kombe la Washindi barani Afrika, mwaka 1996 na kutolewa na Blackpool ya Zimbabwe. 
    Yosso hao wangeweza kufanya maajabu zaidi, kama si viongozi wakati huo kuendekeza imani za kishirikina na kuacha kuwapa maandalizi bora vijana, kwani wakihitaji ushindi wa 1-0 ili waingie Nusu Fainali kwenye mechi ya nyumbani baada ya kufungwa 2-1 ugenini, walijikuta wakifungwa tena 2-1 nyumbani.
    Mchezaji mmoja wa Yanga alifichua siri kwamba, wachezaji walibughudhiwa usiku kucha kwa mambo ya kishirikina na hawakulala vizuri, matokeo yake wakaamka wamechoka na kufungwa nyumbani.
    Awali, Yanga ilianza vyema kwa kuitoa Vaal Reef Professionals ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-3, ikianza kulazimisha sare ya 2-2 ugenini, kabla ya kushinda 2-1 nyumbani.
    Katika raundi ya pili, Yanga ilikutana na Tamil Cadets Club ya Mauritius na kuitoa kwa jumla ya mabao 4-2, ikishinda ugenini  3-1 na kutoa sare ya 1-1 nyumbani, hivyo kukata tiketi ya Robo Fainali
    Lwandamina ni kocha mzuri, ambaye lakini anaweza kufaa katika kikosi chenye wachezaji wengi vijana wadogo wengi watakaoyapokea mazoezi magumu.
    Lakini kwa Yanga kutaka kumfukuza mapema, tuamini walikurupuka kumleta Lwandamina?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WALIKURUPUKA KUMLETA LWANDAMINA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top