• HABARI MPYA

    Tuesday, January 17, 2017

    YANGA KUIJONGELEA SIMBA NYUMA LEO?

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara, Yanga leo watajaribu kupunguza gepu la pointi dhidi ya vinara, Simba SC kugok nne hadi moja.
    Simba SC inaongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zao 44 baada ya kucheza mechi 18, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 40 za mechi 18 pia.
    Na leo jioni Yanga watashuka Uwanja wa Maji Maji mjini Songea kumenyana na wenyeji, Maji Maji wakihitaji ushindi ili kujisogeza nyuma kabisa ya Simba.
    Kikosi cha Yanga SC kipo Songea tangu juzi jioni baada ya kuwasili kufuatia safari ya kutwa nzima kwa baranara kutoka Dar es Salaam
    Wachezaji watano wanakosekana kwenye kikosi hicho ambao ni beki Vincent Bossou ambaye yuko Gabon na timu yake ya taifa, Togo, mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma na viungo Wazambia Justin Zulu, Obrey Chirwa ambao wote ni majeruhi na Emmanuel Martin aliyekwenda kwenye msiba wa mdogo wake Tanga.
    Lakini uzuri ni kwamba, Kocha Mzambia, George Lwandamina amebeba kikosi kipana kikiongozwa na makipa; Deo Munishi ‘Dida’, Ally Mustafa 'Barthez' na Benno Kakolanya, mabeki Hassan Kessy, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Pato Ngonyani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan.
    Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Juma Mahadhi, Deus Kaseke, Simon Msuva, Yussuf Mhilu, Geoffrey Mwashiuya na washambuliaji Amissi Tambwe, Malimi Busungu na Matheo Anthony. 
    Na baada ya mazoezi jana, Lwandamina leo anatarajiwa kushusha kikosi chenye morali ya ushindi katika harakati za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu, ambao unaelekea kwenda Msimbazi, yalipo makao makuu ya Simba.
    Mbali na kuhitaji ushindi ili kujisogeza jirani na Simba, lakini pia Yanga wanatakiwa kushinda ili kurejesha furaha kwa mashabiki wao, baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
    Yanga ilipewa kipigo cha kukumbukwa cha mabao 4-0 na Azam FC katika mchezo wa mwisho wa Kundi B kabla ya kutolewa kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi wiki iliyopita visiwani Zanzibar.
    Na tangu hapo wapenzi wa Yanga wamekuwa wanyonge mbele ya wapinzani wao na kama si Simba kufungwa 1-0 na Azam FC katika fainali, bao pekee la Himid Mao hali ingekuwa mbaya zaidi kwa wana Jangwani.
    Pamoja na yote, bado Yanga inahitaji ushindi tu leo ili kujirudisha kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA KUIJONGELEA SIMBA NYUMA LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top