• HABARI MPYA

    Friday, January 20, 2017

    ULIMWENGU ATUA LIGI KUU YA SWEDEN MIAKA MIWILI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu anaondoka nchini leo kwenda kukamilisha usajili wake klabu ya AFC Eskilstuna ya Ligi Kuu ya Sweden.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Ulimwengu amesema kwamba baada ya mazungumzo ya awali na klabu hiyo anakwenda kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, ambayo awali ilikuwa inajulikana kama FC Cafe Opera na Vasby United.
    “Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa watu wangu wote wa karibu kama Jamal Kisongo ambao wamekuwa karibu na mimi kwa kipindi chote hiki na kunipa ushauri hadi kufikia maamuzi haya ya kujiunga na timu hii. Tumekataa ofa nyingi sana na kuikubali hii kwa sababu za msingi sana,”alisema.
    Thomas Ulimwengu anakwenda kukamilisha usajili wake klabu ya AFC Eskilstuna ya Ligi Kuu ya Sweden

    Ulimwengu alisema kwamba anashukuru Mungu ndoto zake za kucheza Ligi Kuu Ulaya zinatimia na ataitumia AFC Eskilstuna kama daraja la kupandia timu kubwa barani humo.
    “Kila kitu ni malengo tu, inategemea na mtu unataka kitu gani katika wakati gani, nakwenda AFC Eskilstuna kucheza mpira kama nilivyocheza TP Mazembe ili nionekane nisogee mbele zaidi,”alisema.
    Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya Athletic FC ya Sweden, alikocheza hadi 2011 TP Mazembe alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
    Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
    Ulimwengu anajivunia kushinda mataji makubwa akiwa na  Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ULIMWENGU ATUA LIGI KUU YA SWEDEN MIAKA MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top