• HABARI MPYA

  Wednesday, January 18, 2017

  SIMBA YAPUNGUZWA KASI, SARE 0-0 NA MTIBWA

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  SIMBA imepunguzwa kasi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji, Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
  Matokeo hayo yanayoiongezea kila timu pointi moja, yanaifanya Simba ifikishe pointi 45 baada ya kucheza mechi 19 na sasa wanawazidi kwa pointi mbili tu, mabingwa watetezi, Yanga SC. 
  Kipindi cha kwanza Mtibwa Sugar walionekana kucheza kwa kujihami zaidi na kushambulia kwa kushitukiza ili kuwadhibiti wageni wao.
  Kipa wa Simba, Daniel Agyei alidaka shuti kali la mshambuliaji Rashid Mandawa aliyeunganisha krosi ya Henry Joseph dakika ya nane.
  Simba wakajibu shambulizi hilo na dakika nane baadaye, kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohammed akadaka shuti kali la beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
  Agyei akadaka tena shuti kali la mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Jaffar Salum aliyeunganisha krosi ya Haroun Chanongo dakika ya 17.
  Mshambuliaji Mrundi wa Simba, Laudit Mavugo akakaribia kufunga dakika ya 21 baada ya kuitokea vizuri krosi ya kiungo Mghana, James Kotei na kuunganisha kwa kichwa langoni mwa Mtibwa, lakini kipa Said Mohammed akadaka.
  Simba ilipoteza nafasi nyingine mbili za kufunga baada ya Mavugo kupaisha juu katika dakika za 36 na 40 na kipindi cha poli akatolewa baada ya dakika tisa kumpisha Ibrahim Hajib.
  Winga Shiza Kichuya alishindwa kuunganisha krosi ya Nahodha Jonas Mkude dakika ya 56 kwa kupiga nje na dakika ya 73 kipa wa Simba, Agyei akadaka shuti la Rashid Mandawa na kuinyima Mtibwa Sugar bao.
  Refa Emmanuel Mwandembwa wa Arusha alimaliza mpira huo baada dakika tano za nyongeza kufuatia kutimu kwa dakika 90 za kawaida, huku mashabiki wa Mtibwa wakifurahia na wa Simba wakiondoka kwa unyonge uwanjani.
  Kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Said Mohamed, Ally Shomary, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Henry Joseph, Salim Mbonde, Shaaban Nditi, Haruna Chanongo, Ally Makarani, Rashid Mandawa, Jaffary Salum/Hussein Javu dk84 na Vicent Barnabas/Kevin Friday dk78. 
  Simba SC; Daniel Agyei, Hamadi Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Method Mwanjali, Abdi Banda, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Jamal Mnyate dk82, James Kotei, Juma Luizio, Laudit Mavugo/Ibrahim Hajib dk54 na Mwinyi Kazimoto/Pastory Athanas dk75.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAPUNGUZWA KASI, SARE 0-0 NA MTIBWA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top