• HABARI MPYA

    Tuesday, January 10, 2017

    SIMBA YAITOA YANGA KWA MATUTA, KUCHEZA NA AZAM FAINALI

    Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
    SIMBA SC imefanikiwa kwenda fainali ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuwatoa watani wa jadi, Yanga kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Amaan, Zanzibar. 
    Penalti za Simba zilifungwa na Nahodha Jonas Mkude, kipa Daniel Agyei, Muzamil Yassin na beki Mkongo Janvier Besala Bokungu, wakati kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ aliokoa mkwaju wa beki Mzimbabwe Method Mwanjali.
    Waliofunga penalti za Yanga ni Simon Msuva na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko wakati kipa Mghana wa Simba, Daniel Agyei aliokoa penalti za Dida na Mwinyi Hajji Mngwali.
    Kipa Mghana wa SImba, Daniel Agyei amekuwa shujaa leo kwa kuokoa penalti za Dida na Mwinyi Hajji Mngwali

    Simba sasa itakutana na Azam FC Ijumaa katika Fainali. Azam imeitoa Taifa Jang’ombe katika mchezo uliotangulia jioni ya leo.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa visiwani hapa, Mfaume Ali Nassor, aliyesaidiwa na washika vibendera Mgaza Ally na Mbaraka Haule, Waziri Sheha mezani chini ya usimamizi  wa Ramadhan Nassor, timu zote zilishambuliana kwa zamu.
    Pamoja na kuonekana kuingia uwanjani, kinyonge baada ya kufungwa 4-0 na Azam FC Jumamosi katika mchezo wa mwisho wa kundi A, lakini Yanga ilifanikiwa kuwazima wapinzani wao, Simba katika dakika 45 za kipindi kwanza.
    Yanga ndiyo waliokuwa wa kwanza kulitia majaribu lango la Simba dakika ya nane, baada ya Nahodha Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima, raia wa Rwanda kupiga shuti kali akiwa nje kidogo ya 18 lililodakwa na kipa Mghana Daniel Agyei. 
    Yanga tena wakalijaribu lango la Simba dakika ya 15, baada ya winga Simon Msuva kupiga mpira uliorudi kufuatia pigo la mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe kuokolewa, lakini kipa Agyei akaokoa tena akishirikiana na beki Method Mwanjali.
    Simba wakajibu dakika ya 16 baada ya kiungo Mohammed Ibrahim kupiga shuti kali lililodakwa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.
    Msuva tena akakaribia kufunga dakika ya 36 baada ya kumtoka kwa chenga nzuri beki wa kulia wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na kumlamba chenga ya mpira wa kichwa kipa Agyei, lakini alipobinuka ‘kibaiskeli’ kwa pigo dhaifu lililokuwa linaelekea nyavuni, beki Janvier Besala  Bokungu akatokea na kuokoa.
    Z⁠⁠⁠ikiwa zimesalia dakika mbili mpira kuwa mapumziko, mshambuliaji Juma Luizio aliyesajiliw akwa mkopo Desemba kutoka Zesco Unted ya Zambia akaikosesha Simba bao la wazi zaidi dakika ya 43 baada ya kupiga nje mpira uliorudi kufuatia shuti la Mo Ibrahim kugonga mwamba.
    Jonas Mkude alifungua biashara nzuri kwa kupiga penalti ya kwanza ya Simba leo

    Kwa ujumla timu zote zilishambuliana kwa zamu, lakini Yanga ndiyo waliomiliki mpira zaidi wakicheza kwenye eneo lao na kuvusha upande wa pili kwa mipira mirefu, hivyo kuwafanya viungo wa Simba muda mwingi wawe wazurulaji katikati ya Uwanja.
    Mabeki wa pembeni wa Yanga, Mwinyi Hajji Mngwali na Juma Abdul Jaffar wote walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa wameonyeshwa kadi za njano sawa na beki wa Simba, Abdi Banda.
    Kipindi cha pili, Yanga walikianza vizuri pia na kufanikiwa kupata kona dakia 47, ambayo hata hivyo ilipigwa ovyo na Niyonzima na kuokolewa kwa urahisi. 
    Dakika ya 49 Mo Ibrahim akipiga shuti lililodakwa na Dida na dakika ya 52, Simba wakapiga kona mbili mfululizo, ya kwanza Shiza Kichuya na nyingine James Kotei na zote zikaokolewa.
    ⁠⁠⁠⁠⁠⁠⁠Dakika ya 54 Kichiya akapiga tena kona mbili mfululizo na ya mwisho ikaokolewa na beki Kevin Yondan.
    Beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ alitaka kujifunga dakika ya 55 baada ya kupiga fyongo na mpira ukawa unaeleka langoni mwake, kabla ya Yondan kutokea na kuokoa na kuwa kona iliyopigwa na Kichuya, lakini Dida akadaka.
    Yanga ikazinduka dakika ya 78 na winga Emmanuel Martin aliyetokea benchi kipindi cha pili akawapangua mabeki wa Simba na kiungo Jonas Mkude na kupiga shuti lililodakwa na kipa Agyei.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; ⁠⁠Daniel Agyei, Janvier Bokungu, MOhammed Hussein 'Tshabalala', Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Jamal Mnyate dk72, James Kotei, Juma Luizio/Pastory Athanas dk77, Muzamil Yassin na Mohamed Ibrahim/Laudit Mavugo dk85.
    Yanga SC; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Saidi Juma ‘Makapu’, Simoni Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima na Deusi Kaseke/Emmanuel Martin dk63.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAITOA YANGA KWA MATUTA, KUCHEZA NA AZAM FAINALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top