• HABARI MPYA

  Sunday, January 15, 2017

  SIMBA SC TAYARI WAPO MORO KWA SHUGHULI NA MTIBWA SUGAR JUMATANO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Simba SC tayari kipo Morogoro baaada ya kuondoka leo mchana kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mtibwa Sugar Jumatano.
  Ikitoka kulikosakosa Kombe la Mapinduzi baada ya kufungwa 1-0 na Azam FC katika fainali usiku wa Ijumaa Uwanja wa Amaan, Zanzibar bao pekee la kiungo Himid Mao Mkami kwa shuti kali – Simba itajaribu kuendelea kufanya vizuri katika Ligi Kuu Jumatano.
  Kwa sasa, Wekundu hao wa Msimbazi ndiyo wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 44 za mechi 18, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 40 za mechi 18 pia.
  Yanga wenyewe watakuwa wageni wa Maji Maji Uwanja wa Maji Maji mjini Songea kesho katika mfululizo wa ligi hiyo.   
  Juzi Kocha msaidizi wa Simba SC, Mganda Jackson Mayanja alisema kwamba baada ya kushindwa kutwaa Kombe la Mapinduzi sasa wanahaimshia nguvu zao zote kwenye Ligi Kuu.
  Mayanja alisema kwamba wanata wasifanye makosa katika mechi zao za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kuhakikishia hawapotezi mechi hata moja, ili watimize dhamira ya kutwaa ubingwa.  
  “Mbali na kufungwa lakini wachezaji wetu walicheza mpira mzuri na baaada ya kuondolewa katika michuano hiyo tunaelekeza nguvu zetu katika Ligi Kuu kuhakikisha hatushuki kileleni hadi tunatwaa ubingwa,”alisema Mayanja.
  Simba juzi usiku ilishindwa kutwaa Kombe la Mapinduzi 2017, baada ya kufungwa 1-0 na Azam Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Hilo linakuwa taji la tatu la Kombe la Mapinduzi kwa Azam FC baada ya awali kutwaa katika miaka ya 2012 na 2013, hivyo kufikia rekodi ya Simba waliokuwa wanaongoza kwa kutwaa mara nyingi katika miaka ya 2008, 2011 na 2015. 
  Sifa zaidi kwa Kocha aliyeiongoza Azam katika mashindano haya, Iddi Nassor ‘Cheche’ baada ya kufukuzwa kwa Waspaniola chini ya Zeben Hernandez Rodriguez ambaye ameweka rekodi ya kutofungwa hata bao moja.
  Azam pia imeendeleza rekodi yake ya kuchukua Kombe hilo mara zote ilizoingia, wakati kwa Simba hii ni mara ya tatu wanaingia fainali bila kuchukua Kombe kama mwaka 2012 na 2014.
  Ushindi huo Azam walizawadiwa Sh. Milioni 10 na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, wakati Simba walipata Sh. Milioni 5.
  Kipa Bora wa Mashindano ni Aishi Manula, Beki Bora ni Mzimbabwe Method Mwanjali wa Simba na Mfungaji Bora ni Simon Msuva wa Yanga.
  Katika Ligi Kuu, Simba SC ndiyo wanaongoza kwa pointi zao 44 za mechi 18, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 40. Simba watashuka dimba Jumatano jioni kumenyana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi kitaondoka kesho kwenda Moro.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC TAYARI WAPO MORO KWA SHUGHULI NA MTIBWA SUGAR JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top