• HABARI MPYA

    Friday, January 13, 2017

    SAMATTA: SIASA ZIKIWEKWA KANDO STARS ITAFUZU AFCON 2019

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba siasa zikiwekwa kando wanaweza kurejea kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019.
    Taifa Stars imepangwa Kundi L kufuzu AFCON mwaka 2019 nchini Cameroon pamoja na timu za Uganda, Cape Verde na Lesotho katika droo iliyopangwa jana usiku mjini Libvreville, Gabon, zinapofanyika fainali za mwaka huu.
    Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo kwa simu kutoka Genk, Ubelgiji, Samatta alisema kwamba wamebahatika kupangwa katika kundi jepesi ambalo kama maandalizi yatakuwa mazuri Stars itafanikiwa kufuzu.
    Mbwana Samatta (kushoto) amesema kwamba siasa zikiwekwa kando Taifa Stars inaweza kurejea AFCON mwaka 2019

    “Nadhani ni kundi saizi yetu kabisa, katika vipindi vyote tulivyopitia sisi, kwa sasa tupo katika kundi ambalo siasa zikiwekwa kando Tanzania ina nafasi ya kufanikiwa,”alisema Samatta aliyeanza kuchezea Taifa Stars mwaka 2012 chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen.
    Mshambuliaji huyo wa KRC Genk ya Ligi Kuu Ubelgiji ametimiza mwaka mmoja tangu arithi beji ya Nahodha wa Taifa Stars kutoka kwa beki wa Yanga ya nyumbani, Tanzania, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ chini ya kocha mzalendo, Charles Boniface Mkwasa.
    Tanzania imeshiriki mara moja tu AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria tena wakati huo bado zikiitwa Fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika. Na mwaka huo, Taifa Stars iliyopangwa Kundi A pamoja na wenyeji Super Eagles, Mafarao wa Misri na Tembo wa Ivory wa Coast, ilishika mkia baada ya kufungwa mechi mbili 3-0 na Nigeria, 2-1 na Misri na 1-1 na Ivory Coast.  
    Majirani, Kenya pia wataanzia hatua ya makundi, wakiwa wamepangwa Kundi F pamoja na Ghana, Ethiopia na Serra Leone, wakati Rwanda ipo Kundi H pamoja na Ivory Coast, Guinea na Afrika ya Kati (CAR).
    Michuano hiyo itaanzia kwa hatua ya mchujo, Raundi ya Awali itakayohusisha timu za Comoros, Djibouti, Madagascar, Mauritius, Sao Tome E Principe na Sudan Kusini.
    Timu zitakazofuzu hapo zitaingia moja kwa moja kwenye makundi A, B na C kukamilisha idadi ya timu nne nne. Kundi A lina timu za Senegal, Equatorial Guinea na Sudan, B kuna wenyeji Cameroon, Morocco na Malawi na C kuna Mali, Gabon n Burundi.
    Makundi mengine ni; D: Algeria, Togo, Benin na Gambia, E: Nigeria, Afrika Kusini, Libya na Shelisheli,
    G: DRC, Kongo, Zimbabwe na Liberia, I: Burkina Faso, Angola, Botswana na Mauritania, J: Tunisia, Misri, Niger na Swaziland, K: Zambia, Msumbiji, Guinea-Bissau na Namibia.
    Mshindi wa kila kundi atafuzu moja kwa moja AFCON ya 2019, wakati timu nyingine tatu zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zaidi ya nyingine zitafuzu kama washindi wa pili bora. 
    Cameroon ikiongoza Kundi, mshindi wa pili atafuzu moja kwa moja na kama itashika nafasi ya tatu au ya nne, mshindi wa kwanza atafuzu moja kwa moja na mshindi wa pili atawania nafasi tatu za ziada za kufuzu kama mmoja wa washindi wa pili bora. 
    Hatua ya mchujo itachezwa kati ya Machi 20 na 28 wakati mechi za kwanza za makundi zitaanza Juni 5 na 13, mwaka huu za pili Machi 19 na 27, mwaka 2018, za tatu Septemba 3 na 11, mwaka 2018 za nne Oktoba 8 na 16, mwaka 2018 na za tano Novemba 5 na 13, mwaka 2018.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA: SIASA ZIKIWEKWA KANDO STARS ITAFUZU AFCON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top