• HABARI MPYA

  Tuesday, January 10, 2017

  NI SIMBA, AU YANGA LEO ZANZIBAR?

  Na Mwandishi wetu, ZANZIBAR
  MIAMBA ya soka ya Tanzania, Simba na Yanga inakutana katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi usiku wa leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Mchezo huo wa wapinzani wa jadi katika soka ya Tanzania unatarajiwa kuanza Saa 2:15 usiku na utakuwa wa kwanza kuzikutanisha timu hizo visiwani humo baada ya miaka sita.
  Mara ya mwisho Simba na Yanga kucheza visiwani humo ilikuwa ni Januari 12, mwaka 2011 kwenye fainali ya michuano hiyo hiyo ya Kombe la Mapinduzi.
  Katika mchezo huo, Simba waliibuka na ushindi wa 2-0 mabao ya Mussa Hassan Mgosi dakika ya 33 na Shijja Hassan Mkinna dakika ya 71.
  Kwa ujumla Simba na Yanga zimekutana mara nne hadi sasa kwenye ardhi ya Zanzibar na Yanga imeshinda mara moja mwaka 1975 kwenye fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mabao 2-0 ya Sunday Manara na Gibson Sembuli (marehemu).
  Mechi nyingine zote Yanga wamefungwa na mbali na hiyo ya 2011 ya Mapinduzi, walifungwa kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1, Simba wakitangulia kwa bao la Hussein Marsha na wao kusawazisha kwa bao la Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu) na Nusu Fainali ya Ligi ya Muungano 1-0, bao pekee la Damian Kimti zote mwaka 1992.
  Yanga inaingia kwenye mchezo wa leo, ikitoka kufungwa 4-0 na Azam FC katika mechi ya mwisho ya Kundi A Jumamosi, wakati Simba ilishinda 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys Jumapili.
  Wazi Simba wanaingia kwenye mchezo wa leo wakiwa katika mazingira mazuri kushinda, dhidi ya wapinzani wao ambao dhahiri kipigo cha Azam kiliwavuruga.
  Mambo mawili yalielezwa kusababisha kipigo cha 4-0 cha Yanga kutoka Azam, kwanza ni kuidharau mechi hiyo baada ya mwanzo mzuri na kufuzu mapema Nusu Fainali na pili madai kwamba kocha Lwandamina aliwayafanyisha wachezaji mazoezi magumu asubuhi ya mchezo huo.
  Lakini kilichoonekana uwanjani ni Yanga kuzidiwa, hususan katikam safu ya kiungo ambako wachezaji wake ‘watu wazima’ akina Justin Zulu, Haruna Niyonzima na Thabani Kamusoko walishindwa kumudu kasi ya vijana wadogo akina Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Joseph Mahundi na Stephan Mpondo.
  Zaidi ya hapo, mchezaji tegemeo katika mashambulizi, Simon Msuva hakuwa katika ubora wake na haikuwa ajabu Yanga kuzidiwa siku hiyo.  
  Simba wako vizuri hakuna shaka, japokuwa itaendelea kumkosa Muivory Coast Frederick Blagnon, mshambuliaji mpya Juma Luizio yuko vizuri sawa na Laudit Mavugo aliyefunga mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys.
  Vikosi vinatarajiwa kuwa; Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Juma Luizio na Mohammed Ibrahim.
  Yanga SC; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Geoffrey Mwashiuya, Deus Kaseke na Emmanuel Martin. 
  Pamoja na yote, dakika 90 zitaamu. Ni Simba, au Yanga?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI SIMBA, AU YANGA LEO ZANZIBAR? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top