• HABARI MPYA

  Saturday, January 21, 2017

  YANGA KAZINI NA ASHANTI UNITED KOMBE LA ASFC LEO UHURU, KESHO SIMBA NA POLISI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Yanga SC leo wanaanza kutetea Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kumenyana na Ashanti United Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Wakati Yanga inaanzia hatua hiyo ya 32 Bora pamoja na timu nyingine zote za Ligi Kuu kwa mujibu wa kanuni, Ashanti yenyewe imefika hapa baada ya kuitoa timu ngumu ya Daraja la Kwanza, Friends Rangers.  
  Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa 1-0 ugenini katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Maji Maji Jumanne Uwanja wa Maji Maji mjini Songea.
  Kocha Mzambia, George Lwandamina atampokea tena kikosini mwake, winga Emmanuel Martin ambaye alimkosa kwenye mchezo uliopita kutokana na kwenda kwenye msiba wa kaka yake Tanga.
  Lakini kocha huyo wa zamani wa Zesco United na timu ya taifa ya Zambia, ataendelea kumkosa mshambuliaji wake tegemeo, Donald Ngoma ambaye akiwa anatoka kupona maumivu ya goti, amepata msiba na amesafiri kwenda kwao, Zimbabawe.
  Pamoja na hao, Lwandamina ataendelea kuwakosa pia viungo Wazambia wenzake, Juatin Zulu na Obrey Chirwa ambao wote bado ni majeruhi.
  Vigogo wengine, Simba SC watashuka Uwanja wa Uhuru kesho kumenyana na Polisi Dar es Salaam, wakati washindi wa pili wa mwaka jana, Azam FC watamenyana na Cosmopolitan Jumatatu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa juzi jioni na TFF, mechi nyingine za leo ni kati ya Alliance na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Maji Maji na Mighty Uwanja Maji Maji, Songea, wakati Jumapili mbali na Simba na Polisi Dar, Ruvu Shooting itamenyana na Kiluvya United Uwanja Mabatini, Toto Africans na Mwadui Uwanja wa CCM Kirumba na Mbeya Worriors na Prisons Uwanja Sokoine, Mbeya. 
  Mbali na Azam na Cosmo, mechi nyingine za Jumatatu ni kati ya Stand United na Polisi Mara Uwanja Karume, Musoma, Ndanda FC na Mlale JKT Uwanja Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, wakati Jumanne Mtibwa Sugar watamenyana na Polisi Moro Uwanja wa Uwanja Jamhuri, Morogoro, Kurugenzi FC na JKT Ruvu Uwanja wa Mafinga, Mbeya City na Kabela City Uwanja Sokoine, Madini na Panone Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
  Hatua ya 32 Bora itakamilishwa kwa mechi mbili Jumatano, Singida United wakiikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Namfua, Singida na African Lyon na Mshikamano Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Hata hivyo, mchezo wa Lyon na Mshikamano unaweza kusogezwa mbele ikibidi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KAZINI NA ASHANTI UNITED KOMBE LA ASFC LEO UHURU, KESHO SIMBA NA POLISI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top