• HABARI MPYA

  Friday, January 20, 2017

  MANE AIPELEKA SENEGAL ROBO FAINALI AFCON, ALGERIA WADUNDWA

  SENEGAL imekuwa timu ya kwanza kwenda Robo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuifunga 2-0 Zimbabwe katika mchezo wa Kundi B jana mjini Franceville, Gabon.
  Mabao ya Senegal usiku wa jana yalifungwa na nyota wa Liverpool, Sadio Mane dakika ya tisa na Henri Saivet dakika ya 14.
  Na kwa ushindi huo, Senegal inafikisha pointi sita baada ya kucheza mbili, hivyo kujihakikishia kutinga Robo Fainali ya AFCON ya 2017 hizi zikiwa dalili kwao baada ya muda mrefu.
  Tangu washike nafasi ya nne mwaka 2006, Senegal wamekuwa wakisota kwenye michuani hiyo na kushindwa kuvuka hatua ya makundi mara tatu na kutofuzu kabisa mara mbili.
  Sasa wana uhakika wa kuongoza Kundi B kwa matokeo yoyote ya mchezo wao wa mwisho na Algeria Jumatatu ijayo.
  Mchezo mwingine wa kundi hilo jana, Tunisia iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Algeria na kujiwekea mazingira ya kufuzu robo Fainali.
  Mechi yao ya mwisho ya kundi hilo dhidi ya Zimbabwe mjini Libreville itachezwa muda mmoja na mechi kati ya Senegal na Algeria.
  Mabao ya Tunisia yalifungwa na Aissa Mandi aliyejifunga dakika ya 50 na Naim Sliti kwa penalti dakika ya 66, wakati la Algeria lilifungwa na Sofiane Hanni dakika ya 90.
  Michuano hiyo itaendelea leo kwa mechi mbili za Kundi C, mabingwa watetezi, Ivory Coast wakimenyana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Saa 1:00 usiku na Morocco wakimenyana na Togo Saa 4:00 usiku.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MANE AIPELEKA SENEGAL ROBO FAINALI AFCON, ALGERIA WADUNDWA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top