• HABARI MPYA

  Friday, January 06, 2017

  MAHREZ MWANASOKA BORA AFRIKA, ONYANGO AMRITHI SAMATTA

  HISTORIA imeandikwa usiku wa jana jana ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa mjini Abuja baada ya winga wa Algeria na Leicester City Riyad Mahrez kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika Year 2016.
  Kipa wa Uganda, Denis Onyango naye ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika 2016.
  Mahrez, mwenye umri wa miaka 25, anakuwa Mualgeria wa kwanza kushinda tuzo hiyo tangu ianzishwe na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwaka 1992.
  Mchezaji huyo ambaye alitoa mchango mkubwa kwa klabu yake, Leicester City kutwaa taji la Ligi Kuu ya England msimu uliopita na Algeria kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka huu Gabon, alipata kura 361 kushinda tuzo hiyo.
  Amewashinda mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon aliyekuwa anashikilia tuzo hiyo ambaye alipata kura 313, wakati mshambuliaji Msenegali, Sadio Mane amekuwa wa tatu kwa kura zake 186.
  Riyad Mahrez ndiye Mwanasoka Bora wa Mwaka 2016 Afrika  

  Ikumbukwe mshindi anachaguliwa kwa kura za Makocha Wakuu au Wakurugenzi wa Ufundi wa vyama na mashirikisho ya soka wanachama wa  CAF, wajumbe wa Kamati ya vyombo vya Habari ya CAF, Wajumbe wa Kamati ya Ufundi na Maendeleo ya CAF na jopo la wataalamu 20.
  Katika tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrikan, Onyango pia ameweka historia ya kuwa kipa wa kwanza kushinda na kuifanya iendelee kubaki Afrika Mashariki baada ya mwaka jana kuchukuliwa na Mtanzania, Mbwana Samatta.  
  Kipa huyo mwenye umri wa miaka 31 ambaye aliipa Uganda tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39, na pia akaipa Mamelodi Sundowns taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana, alipata kura 252, 24 zaidi ya mchezaji mwenzake wa klabu, Khama Billiat wa Zimbabwe, huku Mzambia Rainford Kalaba akipata kura 206 katika nafasi ya tatu.
  Mshambuliaji wa Nigeria, Asisat Oshoala ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike akiwabwaga Gabrielle Aboudi-Onguene wa Cameroon na Elizabeth Addo wa Ghana, hiyo ikiwa tuzo yake ya pili baada ya mwaka 2014 mjini Lagos.
  Na kwake, ilikuwa furaha ya pili usiku wa jana baada ya timu ya taifa ya wanawake ya Nigeria, Super Falcons kushinda tuzo ya Timu Bora ya Taifa ya Wanawake ya Mwaka baada ya kutwaa taji la nane la Kombe la Mataifa ya Afrika la Wanawake nchini Cameroon mwezi Desemba 2016.
  Habari njema zaidi kwa Nigeria ni washambuliaji wake wawili, Kelechi Iheanacho na Alex Iwobi kushinda Tuzo za Mchezaji Bora Anayechipukia na Mchezaji Bora Kijana wa Mwaka.
  Tuzo mbili zaidi zilikwenda kwa Sundowns, kama Klabu Bora ya Mwaka na Kocha wake Mkuu, Pitso Mosimane kama Kocha Bora wa Mwaka.
  Timu ya taifa ya Uganda, The Cranes kwa kufuzu AFCON ya kwanza baada ya miaka 39 imeshinda tuzo ya timu bora ya Taifa ya Mwaka.
  refa wa Gambian, Bakary Papa Gassama ameshinda tuzo ya Refa Bora wa Mwaka kwa mara ya tatu mfululizo na kufuatia Guinea Bissau kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka huu Gabon, Manuel Lopes Nascimento, Rais wa Shirikisho la Soka Guinea Bissau ameshinda tuzo ya Kiongozi Bora wa Mwaka.
  Mkali wa zamani wa mabao wa Ivory Coast, Laurent Pokou, aliyefariki dunia Novemba mwaka jana alitunukiwa tuzo y Gwiji wa Afrika kwa pamoja na Mcameroon, Emilienne Mbango mwasisi wa soka la wanawake Cameroon.
  Wakati bado soka ya wanawake haijachipua Cameroon, Mbango alikuwa anacheza na Roger Milla alipokuwa klabu ya Leopards Douala miaka ya sabini.
  Tuzo hizo zilipambwa na burudani ya wanamuziki nyota barani Femi Kuti, Flavour, Yemi Alade na Omawumi wate wa Nigeria, Muffinz wa Afrika Kusini na Diamond Platinumz wa Tanzania.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAHREZ MWANASOKA BORA AFRIKA, ONYANGO AMRITHI SAMATTA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top