• HABARI MPYA

  Thursday, January 19, 2017

  KIUNGO MWENYE KIPAJI MTANZANIA ATUA ZANACO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIUNGO mshambuliaji chipukizi wa Tanzania, Ayubu Reuben Lyanga ameondoka juzi nchini nchini kwenda Lusaka, Zambia kujiunga na mabingwa wa nchini humo, Zanaco FC.
  Hiyo inafuatia kocha Mkuu wa timu hiyo, Numba Mumamba kumjaribu na kuridhishwa naye mchezaji huyo mwenye kipaji na kasi, hivyo kuamua kumpa nafasi.
  Meneja wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba  Lyanga alikuwa Zanaco kwa majaribio akafuzu na kusajiliwa kabla ya kurejea nyumbani kuaga na kwenda tena Lusaka kuanza rasmi maisha mapya.
  “Kwa kweli Lyanga ni mchezaji mwenye kipaji ambaye binafsi nina matumaini naye sana kwamba anaweza kufika mbali, mengine tumuachie Mungu mwenyewe,”alisema Kisongo.
  Mchezaji huyo anayeweza kucheza wingi zote mbili, kulia na kushoto ni mdogo wa mshambuliaji wa zamani wa Coastal Union ya Tanga na Simba SC ya Dar es Salaam, Daniel Lyanga ambaye kwa sasa anachezea Fanja ya Oman.
  Na Kisongo alisema baada ya kuibua kipaji cha mchezaji huyo huko Moshi, akampeleka African Sports ya Tanga kucheza kupata uzoefu kabla ya kumpeleka Zambia.
  “Amecheza Ligi Daraja la Kwanza mzunguko wa kwanza pale African Sports, baada ya kuona sasa amepata uzoefu kidogo ndiyo nimempeleka Zambia akajaribu bahati yake,”alisema.
  Kisongo pia ndiye Meneja wa Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta ambaye kwa sasa anachezea KRC Genk ya Ubelgiji. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIUNGO MWENYE KIPAJI MTANZANIA ATUA ZANACO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top