• HABARI MPYA

  Friday, January 13, 2017

  KIJEBA WA KONGO 'ALIYEWAONEA' SERENGETI BOYS AITWA GABON HARAKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limewapa siku 10 Shirikisho la Soka Kongo (FECOFOOT) kumuwasilisha mchezaji Langa Lesse Bercy mjini Libreville, Gabon afanyiwe vipimo vya MRI ili kuthibitisha umri wake kama anaruhusiwa kucheza mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17.
  Katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya CAF jana mjini Libreville, FECOFOOT wametakiwa kumpeleka mjini humo Langa Lesse Bercy akafanyiwe vipimo kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya zoezi hilo kushindikana mara mbili.
  Langa Lesse Bercy anatakiwa Gabon ndani ya siku 10 ili afanyiwe vipimo

  TFF ilimlalamikia mchezaji huyo baada ya Kongo kuitoa U-17 ya Tanzania katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya fainali za mwaka huu zilizopangwa kufanyika Madagascar.

  Awali, Kongo walitakiwa kumpeleka mchezaji huyo makao makuu ya CAF mjini Cairo, Misri kwa vipimo, lakini mara mbili wakashindwa kufanya hivyo. 
  Wakati huo huo: CAF imeivua uenyeji wa fainali za U-17 AFCON 2017 na imetoa muda hadi Januari 30 mwaka huu nchi nyingine kujitokeza kuomba uenyeji.
  Hiyo inafuatia ripoti ya Kamati ya Ukaguzi CAF, ambayo ilibaini Madagascar hawajakamilisha mambo mengi. 
  Tanzania, walioomba kufanya fainali za 2019 wanaweza kupewa yenyeji wa fainali za mwaka huu iwapo watakuwa tayari. 
  Katika hatua nyingine, Kamati ya Utendaji ya CAF, imemteua Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Chilla Tenga kuwania nafasi ya Uwakilishi kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza, akichuana na Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Zambia, Kalusha Bwalya na Kwesi Nyantakyi wa Ghana.
  Tarek Bouchamaoui wa Tunisia anawania Ujumbe wa FIFA kwa zinazozungumza lugha za Kiarabu, Kireno na Kihispaniola, Constant Omari Selemani wa DR Congo na Augustin Sidy Diallo wa Ivory Coast wanawania kwa upande wa nchi zinazozungumza Kifaransa.
  Almamy Kabele Camara (Guinea), Chabur Goc (South Sudan), Danny Jordaan (Afrika Kusini), Hani Abo Rida (Misri) na Lydia Nsekera (Burundi) wanawania nafasi moja ya Mwakilishi wa Kike kutoka Afrika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIJEBA WA KONGO 'ALIYEWAONEA' SERENGETI BOYS AITWA GABON HARAKA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top