• HABARI MPYA

    Sunday, January 22, 2017

    JUUKO AWEKA REKODI AFCON JAPO UGANDA YATUPWA NJE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI wa Simba, Juuko Murshid jana amewekaa rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kucheza mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu nchini Gabon.
    Juuko ni kati ya wachezaji watatu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara waliopo AFCON, wengine wakiwa na beki wa Yanga Vincent Bossou wa Togo na winga wa Azam, Bruce Kangwa wa Zimbabwe, ambao hata hivyo wenzake wamekwenda mechi mbili bila kucheza.
    Juuko alikosa mchezo wa kwanza tu Uganda ikifungwa 1-0 na Ghana, lakini jana alikuwepo uwanjani kwa dakika zote 90, The Cranes ikichapwa 1-0 tena na Misri.
    Bao hilo la Abdallah El Said dakika ya 89 linaitupa nje Uganda na sasa wataingia kwenye mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mali kukamilisha ratiba tu.
    Katika mchezo uliotangulia jana, mshambuliaji Asamoah Gyan aliipeleka Ghana Robo baada ya kufunga bao pekee dakika ya 21 akimalizia krosi ya Jordan Ayew, Black Stars ikiilaza 1-0 Mali.
    Michuano hiyo inaendelea leo kwa wenyeji Gabon kumenyana na Cameroon katika mchezo wa Kundi A mjini Libreville ambao wanatakiwa lazima washinde ili kwenda Robo Fainali.
    Wakifungwa watatolewa na wakitoa sare itabidi wasikilizie matokeo ya mechi nyingine ya mwisho ya kundi hilo kati ya Burkina Faso na Guinea-Bissau.
    Rais wa Gabon, Ali Bongo aliwatembelea wachezaji jana na kipa Didier Ovono akasema: "Rais ametupa hamasa kuelekea mechi hiyo. Hiyo itakuwa fainali yetu ya kwanza."
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JUUKO AWEKA REKODI AFCON JAPO UGANDA YATUPWA NJE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top