• HABARI MPYA

    Thursday, January 05, 2017

    JERRY MURO AIANGUKIA TFF, AOMBA ASAMEHEWE ARUDI KAZINI YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro ameomba msamaha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  kwa adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka.
    Julai mwaka jana, Muro alifungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3 baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF dhidi yake.
    Katika barua yake kwa TFF, Muro amesema kwamba anakiri kupata barua ya kufungiwa kutoka Kamati ya Maadili, lakini anaomba msamaha baada ya kutumikia nusu ya adhabu yake.
    Jerry Muro ameomba msamaha TFF kwa adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka

    Muro ameomba apunguziwe adhabu na kurudi kutekeleza majukumu yake kwa mwajirin wake, Yanga SC kuanzia kipindi hiki cha michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayoendelea visiwani Zanzibar.  
    Mapema wiki iliyopita, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa mahasimu, Simba SC, Hajji Manara alimuombea msamaha Muro pia. Na Wasemaji wa timu nyingine akiwemo Massau Bwire wa Ruvu Shooting walkimuombea msamaha pia mwenzao huyo, wakiamini atakuwa amejirekebisha. 
    Muro alifungiwa Jukai 8 mwaka jana baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde kilichofanyika mjini Dar es Salaam.
    Makosa yaliyomtia hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi leo.
    Kwa kosa hilo akahukumiwa kutengana na masuala ya soka kwa mwaka mmoja- wakati shitaka lingine lililomtia hatiani ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.

    Katika shitaka hilo, Jerry anadaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba kwenye mchezo huo ambao timu yake ilifungwa 1-0 na Mazembe Juni 28, mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Kwa kosa hilo Jerry Muro alifungiwa mwaka mmoja pia na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3 ingawa adhabu zote zinakwenda sambamba – maana yake atakuwa pembeni na masuala ya soka kwa mwaka mmoja tu.
    Hata hivyo, Jerry Muro alifanikiwa kuishinda TFF katika shitaka la kupingana na maamuzi ya shirikisho hilo juu ya masuala ya utoaji wa haki za matangazo ya Televisheni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JERRY MURO AIANGUKIA TFF, AOMBA ASAMEHEWE ARUDI KAZINI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top