• HABARI MPYA

  Sunday, January 08, 2017

  HIYO NDIYO AZAM YA IDDI CHECHE, HUJAKUTANA NA SIMBA YA OMOG

  KOCHA mpya, Mzambia George Lwandamina jana ameiongoza Yanga katika mchezo wa saba tangu aanze kazi Novemba akirithi mikoba ya Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi.
  Na bahati mbaya kwake, Yanga jana ikapoteza mchezo wa pili yeye kazini, baada ya kufungwa 4-0 na Azam FC Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Ikumbukwe Lwandamina alikaribishwa Yanga kwa kipigo cha 2-0 kutoka kwa JKU ya Zanzibar, mabao yote yakifungwa na kinda Emmanuel Martin ambaye baada ya mechi alisajiliwa na timu ya Jangwani.
  Baada ya kipigo hicho kutoka kwenye mchezo huo wa kirafiki, Lwandamina akashinda mechi tano zilizofuata na sare moja katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Mapinduzi. 
  Yanga ilisinda 2-0 dhidi ya JKT Ruvu, ikatoa sare ya 1-1 na African Lyon, ikashinda 4-0 na Ndanda FC zote Ligi Kuu kabla ye kugeukia Kombe la Mapinduzi ambako ilianza na ushindi wa 
  6-0 dhidi ya Jamhuri kabla ya kuipiga 2-0 Zimamoto na jana yenyewe kulala 4-0 kwa Azam.
  Katika mchezo wa jana, hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’.
  Bocco alifunga bao hilo dakika ya pili tu kwa shuti kali baada ya kuukuta mpira uliopanguliwa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ baada ya shuti kali pia la kiungo Joseph Maundi.   
  Baada ya bao hilo, Yanga walijaribu kufunguka kwa kuongeza mashambulizi, lakini safu ya ulinzi ya Azam ilikuwa madhubuti mno.
  Iliweza kuokoa mipira yote ya kutokea pembeni ya Yanga na hivyo kumnyima mwanya kabisa mshambuliaji hatari wa Yanga, Amissi Joselyn Tambwe.
  Katika dakika zote 45 za kipindi cha kwanza, Yanga haikuwa na shambulizi la kutisha langoni mwa Azam, zaidi ya krosi na kona za kawaida mno, ambazo ziliokolewa kwa urahisi.
  Lakini Bocco angeweza kufunga mabao matatu kama angetumia nafasi nyingine mbili nzuri na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alikosa bao la wazi pia baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga hadi kwenye sita na kupiga pembeni.   
  Kipindi cha pili nyota ya Azam iliendelea kung’ara na kufanikiwa kuvuna mabao matatu zaidi.
  Mshambuliaji Mghana, Yahya Mohammed alifunga bao la pili dakika ya 54 kwa kichwa akimzidi maarifa beki Andrew Vincent ‘Dante’ baada ya krosi ya Sure Boy.
  Mahundi akafunga bao zuri zaidi kwenye mchezo huo dakika ya 80 kwa shuti la umbali wa mita zaidi ya 20 kuipatia Azam bao la tatu baada ya pasi ya Sure Boy.
  Winga Mghana, Enock Atta Agyei aliyetokea benchi kipindi cha pili, akaifungia Azam bao la nne dakika ya 85 akimchambua vizuri kipa Dida baada ya pasi ya Samuel Afful aliyeingia kipindi cha pili pia.
  Kwa ujumla Yanga ilicheza ovyo mno na Azam ingeweza kupata ushindi wa kihistoria kama ingetumia nafasi zaidi ilizotengeneza.  
  Pamoja na kipigo, bahati nzuri kwao Yanga wanakwenda Nusu Fainali kama washindi wa pili wa Kundi A wakimaliza na pointi saba sawa na Azam inayoongoza kwa wastani wa mabao.
  Sasa Azam itacheza na mshindi wa pili wa Kundi B katika Nusu Fainali, wakati Yanga itacheza na mshindi wa kwanza wa kundi hilo.
  Bila shaka, hayakuwa matarajio kabisa ya Lwandamina kukutana na kipigo kikali kama kile na kwa desturi za timu zetu kongwe, Simba na Yanga sasa Mzambia huyo amekalia kuti kavu.
  Wenye timu yao wanasema haijawahi kutokea wao kufungwa 4-0 na Azam, mwisho ilikuwa mabao matatu. Lakini kinachowauma Yanga ni kufungwa na Azam iliyoonekana dhaifu kipindi hiki.
  Na kinachowauma zaidi Yanga kingine ni kufungwa na Azam ambayo iliongozwa na wasimamizi wakati timu ipo kwenye mchakato wa kusaka kocha mpya.
  Ikumbukwe Azam ifukuza makocha wake wote kutoka Hispania, Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Msaidizi wake, Yeray Romero, Kocha wa Makipa Jose Garcia, Kocha wa Viungo, Pablo Borges na Mtaalamu wa tiba za Viungo, Sergio Perez.
  Kocha wa Timu B, Iddi Nassor ‘Cheche’ akapewa timu pamoja na aliyekuwa kocha wa makipa wa timu hiyo, Iddi Abubakar.
  Sasa Yanga wanajiuliza kama Azam ya Cheche inawapiga 4-0, wakikutana na Simba ya Mcameroon, Joseph Marius Omog itakuwaje? Lwandamina kazi anayo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HIYO NDIYO AZAM YA IDDI CHECHE, HUJAKUTANA NA SIMBA YA OMOG Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top