• HABARI MPYA

    Tuesday, January 03, 2017

    DILI LA HAJIB MISRI LAINGIWA UKAKASI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BIASHARA ya mshambuliaji wa Simba SC, Ibrahim Hajib kwenda Haras El Hodoud ya Misri inaelekea kama kutokamilika kwa sasa.
    Dirisha la usajili la Misri lilifungwa juzi na Haras El Hodoud hawakuwa wamefanya mawasiliano yoyote na Simba SC hadi jana jioni.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Sunday Manara alisema jana katika mazungumzo na Bin Zubeiry Sports - Online kwamba klabu yake haijapokea ofa yoyote kutoka kwa Haras El Hodoud.
    “Sijui wanategemea nini, maana dirisha la usajili la kwao linafungwa leo (jana). Sasa sijui wana mpango gani,”alisema Manara.
    Ibrahim Hajib (kushoto) akiwa na wachezaji wa Haras El Hodoud nchini Misri

    Juzi Hajib alisema kwamba amefanya mazungumzo ya awali na Haras El Hodoud na kufikia makubaliano, lakini kwanza wanatakiwa kumalizana na klabu yake ya sasa, Simba SC.
    “Ninamshukuru Mungu nimefurahia siku zangu chache za kuwa Alexandria, nilikuwa katika klabu nzuri, mazingira mazuri na wachezaji wenzangu kule wamenikubali mapema sana. Sasa baada ya yote, ninawasikilizia wao tu ni jinsi gani watalimalizia hili suala,”alisema.
    Hajib alirejea nchini juzi na kusema kwamba atajiunga na timu itakayompa ofa nzuri kati ya Haras El Hodoud ya Misri na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inayomtaka pia.
    Pamoja na kufuzu majaribio na vipimo vya afya Haras El Hodoud, lakini imeripotiwa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini pia inatamaka mchezaji huyo wa Simba kwa kusaini naye mkataba moja kwa moja bila majaribio.
    “Ni kweli nimesikia hizo habari, na si Kaizer tu, timu nyingine kama mbili za Afrika Kusini nazo zimetangaza ofa. Kwanza ninamshukuru Mungu. Mungu ni mkubwa, sasa tusubiri haya maneno yawe vitendo ndiyo tufanye maamuzi,” alisema Hajib.
    Wakala anayeshughulikia mipango ya Hajib nchini Afrika Kusini, Rodgers Mathaba kwa upande wake alikiri juu ya mchezaji huyo kutakiwa na Kaizer Chiefs.
    “Ni kweli, Kaizer wanamtaka Hajib. Najua alikuwa Misri, nasubiri arejee Dar es Salaam nimpigie simu nizungumze naye. Tayari nimekwishazungumza na kocha Steve Khompela wa Kaizer,”alisema.
    Hajib alikuwa ana wiki nzuri ya majaribio Haras El Hodoud ikiwemo kufunga bao moja katika ushindi wa 4-0 kwenye mchezo wa kirafiki Ijumaa.
    Mathaba ndiye aliyempeleka Hajib Afrika Kusini kwa majaribio pia, klabu ya Lamontville Golden Arrows FC ya Ligi Kuu ya ABSA nchini humo na pamoja na kufuzu, wakamtaka arejee Simba kumalizia Mkataba ili baadaye aende kama mchezaji huru. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DILI LA HAJIB MISRI LAINGIWA UKAKASI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top