• HABARI MPYA

  Saturday, January 07, 2017

  AZAM NA YANGA BONGE LA MECHI LEO ZENJI

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  MECHI za Kundi B michuano ya Kombe la Mapinduzi zinahitimishwa leo kwa mchezo kati ya wapinzani wa Tanzania Bara, Azam na Yanga SC utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuanzia Saa 2:30 usiku.
  Mchezo huo utatanguliwa na mechi nyingine ya kundi hilo kati ya Jamhuri ya Pemba na Zimamoto Unguja kuanzia Saa 10:00 jioni.
  Azam inahitaji zaidi ushindi katika mchezo wa leo ili kujihakikishia tiketi ya Nusu Fainali, baada ya kuambuliwa pointi nne katika mechi zake mbili za mwanzo.
  Yanga yenyewe hata sare kwake itafaa kwake, kwani baada ya kushinda mechi zake mbili za mwanzo 6-0 dhidi ya Jamhuri na 2-0 dhidi ya Zimamoto imejikusanyia pointi sita na hazina kubwa ya mabao.
  Mara ya mwisho Azam na Yanga zilitoa sare ya 0-0 Oktoba 16, mwaka jana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 

  Mbali na mahitaji ya kawaida kwa timu zote mbili leo, lakini kikubwa ni upinzani wa asili wa Azam na Yanga zinapokutana timu hizo katika mashindano yoyote.
  Kwa mwaka huu huu utakuwa mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizo, lakini kwa msimu huu ni mechi ya tatu baada ya awali kukutana na mechi ya Ngao ya Jamii Agosti 17, mwaka 2016
  ambayo Azam ilishinda kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2 na Oktoba 16, mwaka jana pia mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ilkiyomalizika kwea sare ya 0-0.
  Mechi zote za awali, Yanga ilikuwa chini ya kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye sasa amekuwa Mkurugenzi wa Ufundi na Azam ilikuwa chini ya Mholanzi, Zeben Hernadez Rordiguez ambaye amefukuzwa Desemba.
  Lakini katika mchezo wa leo, Azam itaongozwa na kocha wa muda, Iddi Nassor ‘Cheche’ anayesaidiwa na Iddi Abubakar na Philip Alando, wachezaji wa zamani wa timu hiyo wakati Yanga itaongozwa na kocha mpya, George Lwandamina, anayesaidiwa na Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na mzalendo Juma Mwambusi.   
  Japokuwa Azam FC inaonekana kuyumba kwa sasa, lakini inatarajiwa tu kutoa upinzani kwa Yanga kama ilivyokuwa kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu zikitoa sare ya 0-0.
  Nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ mwenye bahati ya kuwafunga Yanga anaingia katika mchezo wa leo akiwa vizuri ingawa haijulikani atapangwa pamoja nani pale mbele.
  Kinara wa mabao wa Yanga, Mrundi Amissi Tambwe hajacheza mechi zote mbili za mwanzo za Kombe la Mapinduzi, lakini mshambuliaji mwingine tegemeo la mabao la timu hiyo, Donald Ngoma yuko fiti na amecheza. 
  Mechi ya leo ni kipimo kizuri kwa wachezaji wapya wa kigeni wa Azam, waliosajiliwa dirisha dogo beki Yakubu Mohammed, kiungo Stephan Kingue, washambuliaji Yahaya Mohammed, Samuel Afful na winga Enock Atta Agyei.
  Ni kipimo kizuri kwa wachezaji wapya wa Yanga waliosajiliwa dirisha dogo, kiungo Mzambia Justin Zulu na winga Emmanuel Martin. 
  Vikosi vya leo vinatarajiwa kuwa; Azam FC: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo, Yahaya Mohammed, Samuel Afful na Enock Agyei.
  Yanga SC; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Andrew Vincent ‘Dante’, Justin Zulu, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Emmanuel Martin. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM NA YANGA BONGE LA MECHI LEO ZENJI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top