• HABARI MPYA

  Saturday, December 17, 2016

  YANGA YA LWANDAMINA YAANZA LIGI LEO, SIMBA KESHO MTWARA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BAADA ya mapumziko ya tangu Novemba 10, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mechi za mzunguko wa pili kuanza.
  Mabingwa watetezi, Yanga wataanza na JKT Ruvu Stars Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, mchezo ambao unatarajiwa kuteka hisia za wapenzi wengi wa soka nchini.
  Baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 33, wakizidiwa pointi mbili na vinara, Simba SC – Yanga walibadilisha benchi la Ufundi.
  Aliyekuwa Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm amekuwa Mkurugenzi wa Ufundi, nafasi yake akimuachia Mzambia, George Lwandamina. Lwandamina ameleta Msaidizi wake kutoka Zambia, Noel Mwandila, ingawa waliokuwa Wasaidizi wa Pluijm wanaendelea na kazi.
  Hao ni Meneja Hafidh Saleh, Kocha Msaidizi, Juma Mwambusi, Kocha wa makipa Juma Pondamali pamoja na Datkari Edward Bavu, Mchua Misulu Jacob Onyango na Mtunza Vifaa Mohammed Omar ‘Mpogolo’.
  Benchi hilo jipya la Ufundi la Yanga limekuwa na takriban wiki tatu za kuiandaa timu kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, ikiwemo kupata mchezo mmoja wa kujipima nguvu, ambao walifungwa 2-0 na JKU ya Zanzibar.
  Na baada ya mchezo huo uliofanyika Jumamosi iliyopita, kocha Lwandamina alimsajili mchezaji aliyefunga mabao yote mawili Emmanuel Martin Joseph aliyeanza mazoezi na wenzake juzi.
  Huyo anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa Yanga dirisha dogo baada ya kiungo Mzambia, Justin Zulu wakati pia klabu imemuacha mchezaji mmoja tu, kiungo anayeweza kucheza kama beki pia, Mbuyu Twite aliyedumu Jangwani kwa miaka minne. 
  Na katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa kipa Benno Kakolanya na washambuliaji Malimi Busungu na Matheo Anthony ambao wote ni majeruhi.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mbeya City watamenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mwadui na Toto Africans Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.
  Vinara wa ligi hiyo, Simba wataanza kampeni ya kuwania taji la kwanza baada ya miaka minne kesho kwa kumenyana na Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, wakati Mbao FC watamenyana na Stand United Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, African Lyon na Azam Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Prisons na Maji Maji Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YA LWANDAMINA YAANZA LIGI LEO, SIMBA KESHO MTWARA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top