• HABARI MPYA

    Friday, December 16, 2016

    TFF YAONYA; "WACHEZAJI WENU WA KIGENI HAKUNA KUCHEZA BILA VIBALI VYA UHAMIAJI"

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limezitaka klabu zote zilizosajili wachezaji wa kigeni katika dirisha dogo kutowatumia kwenye mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hadi wapatiwe vibali.
    Taarifa ya TFF kwa vyombo vya Habari leo imesema kwamba klabu hazitakiwi kutumia wachezaji wa kigeni au makocha ambao hawana vibali vya kufanya kazi nchini kutoka Idara ya Uhamiaji. 
    Aidha, TFF pia kwa kutumia kanuni ya 72 ya Ligi Kuu ya Vodacom imezitaka klabu kuhakikisha makocha wake wote wana sifa. 
    Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Kuu ya TFF, kanuni hiyo inasema makocha wanaopaswa kukaa kwenye benchi la Ligi kuu kwa msimu huu wasipungue sifa ya kuwa na leseni B ya CAF.
    Kipa mpya wa Simba kutoka Ghana, Daniel Agyei anahitaji kibali cha Uhamiaji kwanza ili kucheza Ligi Kuu

    "Pia kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza na Pili, masharti ni lazima makocha wawe na sifa za kuzinoa timu hizo ambazo zimeanishwa kwenye kanuni za ligi husika," imesema taarifa ya TFF.
    Duru la Pili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kesho Jumamosi Desemba 17 kwa michezo minne kabla ya michezo mingine minne kufanyika siku ya Jumapili Desemba 18, mwaka huu.
    Katika mechi za kesho, Mabingwa watetezi wa taji hilo, Yanga SC ya Dar es Salaam itakuwa mgeni wa JKT Ruvu ya Pwani kwenye mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Licha ya kwamba mwenyeji wa mchezo huo ni JKT Ruvu ambayo uwanja wake wa nyumbani mara nyingi huwa ni Mabatini ulioko Mlandizi, lakini kwa mujibu wa Kanuni ya 6 (5) na (6) ya Ligi Kuu Bara, mechi zake za nyumbani dhidi ya Simba, Yanga na Azam FC, hufanyika Uwanja wa Uhuru.
    Michezo mingine ya kesho ni Kagera Sugar kuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakati Ruvu Shooting ya Pwani itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani ilihali Mwadui ya Shinyanga itaikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.
    Jumapili, Desemba 18, mwaka huu Mbao FC ya Mwanza itacheza na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakati Ndanda itakuwa mwenyeji wa Vinara wa Msimamo katika Ligi Kuu ya Vodacom, Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
    African Lyon ya Dar es Salaam itaikaribisha Azam FC pia ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru jijijini siku hiyo ya Jumapili wakati Majimaji ya Songea itakuwa Mbeya kucheza na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAONYA; "WACHEZAJI WENU WA KIGENI HAKUNA KUCHEZA BILA VIBALI VYA UHAMIAJI" Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top