• HABARI MPYA

  Friday, December 16, 2016

  NGASSA ASAINI MWAKA MBEYA CITY, AKUTANA NA JUMA SEIF 'KIJIKO'

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  HATIMAYE kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa amesaini klabu ya Mbeya City FC.
  Ngassa alisaini jana mkataba wa mwaka mmoja, kwenye ofisi za City zilizopo jengo la Mkapa Hall, Soko Matola mjini Mbeya, siku ambayo Mbeya City ilimsaini pia kiungo wa zamani wa Yanga, Juma Seif 'Kijiko'.
  Wawili hao wanaungana na wachezaji wengine wapya wanane waliojumishwa kikosini kwenye usajili wa dirisha dogo lililofikia tamati jana Desemba 15.
  Ngassa amekabidhiwa jezi namba 10 iliyokuwa inavaliwa na Joseph Mahundi aliyetimkia Azam FC ya Dar es Salaam kufuatia  kumalizika kwa kandarasi yake.
  Ngassa akisaini mkataba wa mwaka mmoja jana kwenye ofisi za Mbeya City zilizopo jengo la Mkapa Hall, Soko Matola mjini Mbeya 

  Mara baada ya kusaini kandarasi hiyo ya mwaka mmoja Ngassa amesema anataka kufanya kazi kwa kiwango ambacho kitaipa mafanikio timu yake mpya na kuwaziba ‘midomo’ wale wanaamini kwamba soka lake  limefikia  tamati.
  "Najua kuna maneno na minong’ono mingi kuhusu uwezo wangu, muda si mrefu yataisha kwa sababu najua nini nataka kufanya, soka ndiyo maisha yangu, naomba watu wote walio nyuma ya timu hii waniunge mkono nina uhakika tutakuwa na majibu mazuri mwisho wa msimu," alisema.
  Ngassa anasaini akitokea Fanja ya Oman, ambayo aliichezea kwa miezi miwili tu baada ya kujiunga nayo akitokea Free State Stars ya Afrika Kusini alikosajiliwa na kocha wa sasa wa Mbeya City, Kinnah Phiri.
  Kisoka, Ngassa aliibukia Toto Africans ya Mwanza, kabla ya kwenda Kagera Sugar, Yanga SC, Azam FC, Simba na baadaye Jangwani tena.
  Juma Seif 'Kijiko' akisaini mkataba wa mwaka mmoja jana kwenye ofisi za Mbeya City zilizopo jengo la Mkapa Hall, Soko Matola mjini Mbeya

  Wengine waliosajiliwa Mbeya City katika dirisha hili dogo ni Hood Mayanja, Tito Okello, Zahor Pazi, Hussein Salum, Otong William, Raphael Bryson, Daniel Joram, Sameer Abeid na Majaliwa Mbanga.
  Katika  hatua nyiingine kocha Kinnah Phiri  amesema wachezaji, Ramadhani Chombo 'Redondo', Meshack Samuel, Peter Mwangosi, Michael Kerenge, Mackyada Franco, Issa Nelson, Salvatory Nkulula, Hemed Murutabose na Joseph Mahundi aliyemaliza mkataba wake hawatakuwepo tena kwenye kikosi chake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA ASAINI MWAKA MBEYA CITY, AKUTANA NA JUMA SEIF 'KIJIKO' Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top