• HABARI MPYA

    Saturday, December 03, 2016

    MBUYU TWITE KWAHERI YANGA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BEKI anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Junior Twite anahitimisha miaka yake minne ya kuwatumikia vigogo wa Tanzania, Yanga SC baada ya kutua kwa kishindo mwaka 2012 akitokea APR ya Rwanda.
    Mchezaji huyo wa Kongo DR aliyeichezea timu ya taifa ya Rwanda ameachwa na timu ya Jangwani katika usajili huu wa dirisha dogo Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Lakini klabu imepanga kumuaga kwa heshima na huenda ukaandaliwa mchezo maalum wa kumpa mkono wa kwaheri mwezi huu.
    Twite alifanya kituko cha aina yake, baada ya kwanza kusaini Simba Julai 2012 mjini Kigali, Rwanda akiwa mchezaji wa APR, lakini siku chache baadaye akasaini na Yanga kama mchezaji wa St. Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Mbuyu Junior Twite anaondoka Yanga SC baada ya miaka minne tangu apitilize hadi Jangwani, badala ya kusimama Msimbazi

    Na sasa historia ya mchezaji aliyetua kwa utata inafungwa kwa Yanga kuachana na Twite baada ya kumaliza mkataba wake, na nafasi yake inachukuliwa na kiungo Mzambia, Justine Zullu. 
    Zullu anaungana na wachezaji wengine wa kigeni wa Yanga, ambao ni beki Vincent Bossou, viungo Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Obrey Chirwa na washambuliaji Amissi Tambwe na Donald Ngoma.
    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alikwenda Kigali kumsajili Twite na kumpa dola za Kimarekani 30,000 na akafuata taratibu zote hadi kupewa uhamisho wake na Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA).
    Baadaye, mchezaji huyo akasaini Yanga na ikaelezwa alikuwa anacheza kwa mkopo kutoka Lupopo ambao ndiyo walikuwa wana haki ya kumhamisha na si APR. Mwishowe usajili wa Twite kwenda Yanga kutoka Lupopo ndiyo ukapitishwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na si ule wa Simba kutoka APR.
    Hata hivyo, baadaye TFF iliamuru Yanga kurudisha gharama zote za Simba dola 32,000. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBUYU TWITE KWAHERI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top