• HABARI MPYA

    Sunday, December 04, 2016

    KWA NINI MKUDE AWAKWEPE VIONGOZI SIMBA NAYE NI NAHODHA?

    NI jambo la kawaida kwa Ulaya kusikia mapema tu mchezaji fulani hataongeza mkataba atakapomaliza kwa sababu anaondoka.
    Na hilo hutokea wakati mchezaji akiendelea kutekeleza majukumu yake vizuri katika klabu bila kuonyesha tofauti.
    Na hii si kwa Ulaya tu, bali duniani kote hata kwetu Afrika nchi nyingine mambo yako hivyo.
    Mbwana Ally Samatta ni Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania ambaye kwa sasa anachezea KRC Genk ya Ubelgiji aliyojiunga nayo Januari mwaka huu.
    Mapema tu mwaka jana ilijulikana Samatta hataongeza mkataba klabu yake, TP Mazembe ya DRC, lakini aliitumikia kikamilifu hadi siku ya mwisho ya mkataba wake.
    Samatta aliisaidia TP Mazembe kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, naye akawa mfungaji bora ambayo ilimsaidia kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
    Matokeo yake, akaingia Ulaya kwa heshima kubwa ambayo wachezaji wengi wa Kiafrika hawakuingia nayo.
    Aliingia kama Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika, ambayo pia ilimsaidia kumpa heshima ya kupewa nafasi moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza Genk.
    Amefanikiwa kuilinda heshima ya kuwa mchezaji muhimu wa Genk na ameendelea kupandisha kiwango chake.
    Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu ameondoka Mazembe miezi miwili iliyopita baada ya kumaliza mkataba wake, jambo ambalo pia ni mpango wa muda mrefu.
    Mazembe ilijiandaa kuwapoteza Samatta mwaka jana na Ulimwengu mwaka huu kwa kusajili wachezaji wengine mapema na matokeo yake klabu na mchezaji wanaachana vizuri na kutakiana  heri.  
    Kama inavyoripotiwa ni kweli, hapa nchini kiungo Jonas Mkude anawakwepa viongozi wa Simba baada ya kumaliza Mkataba wake.
    Mkude aliteuliwa kuwa Nahodha wa timu mwanzoni mwa msimu huu, kufuatia kustaafu kwa Mussa Hassan Mgosi, ambaye sasa ni Meneja wa timu.
    Mambo mengi hutazamwa kabla ya mchezaji kupewa beji ya Unahodha wa timu, kwa sababu anapewa jukumu la kuwa kiongozi wa wachezaji wenzake ndani na nje ya Uwanja.
    Tulitarajia uongozi wa Simba nao uliyatazama hayo mambo kabla ya kumpa beji Mkude – kwamba atakwenda kufaa kuwa kiongozi wa wachezaji wenzake katika timu.
    Siku zote viongozi huwa wa mwisho kukimbia janga – ili kuwahamasisha wanaowaongoza wavumilie na waweze kukabiliana na hali iliyopo.
    Tulitarajia hata kama kuna tatizo lolote, Mkude angetumia busara na hekima zake za uongozi kwa kutojiruhusu kuwaonyesha picha isiyofaa wachezaji wenzake.
    Mkude amemaliza Mkataba Simba na anatakiwa kuongeza. Anatakiwa kukutana na uongozi kwa mazungumzo juu ya mkataba mpya.
    Lakini inaripotiwa anawakwepa viongozi ambao nao imefikia hatua wamekata tamaa na kuamua kuachana naye. Hii inakuwaje kwa timu na Nahodha wake?
    Kama ni kweli inavyoripotiwa, Mkude anakosea kuwakwepa viongozi wa Simba SC – anapaswa kukutana nao na kuwaambia kilichomo ndani ya nafasi yake.
    Kuna maswali ya kujiuliza hapa, moja; ni kwa nini Mkude anawakwepa viongozi wa Simba wakati tulitarajia suala lake, kubaki au kuondoka lingekuwa linajulikana muda mrefu.
    Tunafahamu Mkude ana mpango wa muda mrefu wa kwenda kucheza soka Afrika Kusini, lakini kwa nini awakwepe viongozi wa Simba wakati anaweza kukutana nao na kuwaambia uamuzi wake?
    Najiuliza maswali kwa sababu Mkude hajatokea kuzungumzia shutuma za kuwakwepa viongozi wa Simba SC kwa kikao cha kuongeza mkataba – hivyo sijui haswa kwa undani kuna nini kati yao?
    Na hiyo ni kwa sababu, wakati mwingine viongozi wa klabu zetu wanakuwa wana mambo magumu kuvumilia.
    Ila kwa vyovyote sioni sababu ya Mkude kuwakwepa viongozi wa Simba aliyoichezea kwa zaidi ya miaka minne sasa, bali anapaswa kukutana nao na kumalizana nao mezani.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA NINI MKUDE AWAKWEPE VIONGOZI SIMBA NAYE NI NAHODHA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top