• HABARI MPYA

    Sunday, December 11, 2016

    KIFO NI MIPANGO YA MUNGU, LAKINI UZEMBE WA KRFA ULICHANGIA PIA

    SOKA ya Tanzania ilipata pigo wiki iliyopita, kufuatia kifo cha Ismail Khalfan wakati anaichezea Mbao FC ya Mwanza katika mechi ya Ligi ya Vijana ya Taira chini ya umri wa miaka 20 Desemba 4, mwaka huu dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera.
    Khalfan alianguka uwanjani dakika ya 74 baada ya kukwatuliwa kidogo na mchezaji mwenzake, lakini hali yake ikawa mbaya ghafla na akalazimika kukimbizwa hospitali kwa gari la Zimamoto kwa kuwa hakukuwa na gari la wagonjwa.
    Inaaminika mchezaji huyo aliyefunga bao la kwanza siku hiyo timu yake ikishinda 2-0 alifariki njiani wakati anakimbizwa hospitali.
    Kwa mara ya kwanza na ya mwisho nilikutana na marehemu Ismail Khalfan Machi mwaka jana nilipokuwa mjini Mwanza na kufika kituo kidogo cha soka, kinachomilikiwa na Mbaki Mutahaba, mdogo wa mmoja wa Wakurugenzi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.
    Mbaki Mutahaba alianzisha kituo chake eneo la Bwiru mjini Mwanza, akianza na vijana wanne tu, ambao alikuwa anawaandaa kuwa wachezaji bora baadaye nchini.
    Mbaki amekodi nyumba maalum eneo la Bwiru ambako Ismail alikuwa anaishi na wenzake watatu, ndani yake ikiwa na gym, darasa la kupata elimu ya shuleni na mahitaji mengine muhimu. 
    Mbali na Ismail, vijana wengine niliowakuta siku hiyo ni Andrea Michael wa Mwanza pia, Boaz Charles wa Manyoni, Singida na Paschal Kibandula wa Ifakara, Morogoro.
    Mkuu wa kituo hicho ni Francis ‘Fura’ Felician, beki wa zamani wa Toto Africans, Pamba za Mwanza, Kagera Stars (sasa Kagera Sugar) ya Bukoba na Sony Sugar ya Kenya.
    Fura amekuwa akiwasimamia watoto hao kuhakikisha wanatekeleza programu zote walizowekewa kuanzia za elimu na mazoezi, tena yeye akiwa ndiye kocha wao Mkuu. 
    Felician mdogo wa mshambuliaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza na Yanga SC ya Dar es Salaam, Fumo Felician alisema kwamba waliwapata watoto hao baada ya kuzunguka kusaka vipaji nchi nzima.
    “Tuna vigezo fulani tulikuwa tunatazama kwa vijana, kama maumbo, uwezo, kipaji na weledi vile vile. Na kwa kuwa uwezo wetu sisi ni mdogo, kwa kuanzia, tukasema tuchukue vijana wanne tu, ila baadaye tukija kupata wafadhili tutaongeza vijana,”alisema Felician. 
    Mkuu huyo wa kituo hicho kinachokwenda kwa jina Football House, amesema watoto hao wanafanya mazoezi na wachezaji wa kituo cha Almasi, maarufu Almasi akademi Uwanja wa sekondari ya Bwiru.
    “Tunachokifanya sisi, hawa vijana mbali ya kuwa na programu zao maalum, lakini baadaye wanachanganyika na vijana wenzao wa Almasi akademi kufanya mazoezi,”alisema.
    Alisema ili kupata uzoefu, vijana hao walisajiliwa na timu ya Almasi akademi ambayo inashiriki Ligi Daraja la Tatu ngazi ya Mkoa wa Mwanza.  
    Fura alisema mradi huo ulianza mwaka 2012, lakini ni mwaka jana ndipo walipokodisha hosteli na kuanza kuwatunza vijana hao na kwamba lengo lao ni kuhakikisha wanacheza Ulaya au Amerika.
    “Hapa ni sehemu ya kuanzia tu, ikitokea hata timu kubwa za hapa baadaye zikavutiwa na vijana wetu kama bado hawajapata nafasi ya kwenda nje, tutawapa kwa makubaliano maalum wawatumie,”alisema Felician.
    Baadaye Ismail alipata mwaliko wa kwenda Marekani kuwania nafasi ya kusoma na kujiendeleza kisoka, ambayo alifanikiwa kuipata.
    Na aliporejea Mwanza kabla ya kwenda Marekani, akaamua kuchezea timu ya vijana ya Mbao FC ili kupata uzoefu zaidi, lakini kumbe ndiyo alikuwa anakielekea kifo chake.
    Inaonekana namna ambavyo safari ya Ismail Khalfan haikuwa ya kubahatisha kisoka, ameanzia mbali na amepitia maisha magumu kwa matarajio ya kutimiza ndoto zake.
    Kifo chake ni pigo kwa kituo cha Mbakhi, familia yake, wazazi wake ambao walikwishaanza kupata picha halisi ya mtoto wao anakoelekea.
    Ninaamini kifo kinapangwa Mungu, lakini nina wasiwasi baadhi ya vifo vinatokana na uzembe wetu au kujisababishia kwa namna yoyote.
    Hakukuwa na gari maalum la wagonjwa uwanjani (Ambulance) wakati mchezo wa Mbao FC na Mwadui unaendelea Uwanja wa Kaitaba na Ismail akakimbizwa hospitali kwa gari la Zimamoto (Fire).
    Kwa kawaida ndani ya Ambulance huwa kunakuwa na mazingira maalum kwa mtu anayekimbizwa hospitali kuendelea kupatiwa huduma ya kwanza njiani – je kwenye Fire?
    Wataalamu wanayajua mambo haya na tukubali pamoja na mipango ya Mungu, lakini uzembe wa Chama cha Soka Kagera (KRFA) kuruhusu mchezo ufanyike uwanjani hakuna gari la wagonjwa ulichangia kifo cha kijana huyo.
    Wakati umefika sasa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lirudi kwenye mstari na kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwenye mchezo wa soka ili kuepuka yenye kuepukika.
    Tumekuwa tukipuuza baadhi ya taratibu kwa sababu husaidia yanapotokea majanga ambayo hayatokei mara kwa mara – lakini tunasahau kwamba kwa kuwa ni taratibu tunapaswa kuzifuata.
    Hata FIFA inaagiza hivyo, Ambulance iwepo uwanjani kabla hadi baada ya mchezo – lakini kwa nini TFF ilipuuza na kwa nini na wao wasibebe lawama kifo cha Ismail? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIFO NI MIPANGO YA MUNGU, LAKINI UZEMBE WA KRFA ULICHANGIA PIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top