• HABARI MPYA

    Thursday, December 01, 2016

    HAJIB VAA MIWANI UIONE JEZI YAKO ULAYA

    Na Dismas Ten, DAR ES SALAAM
    HAKIKA hii ndiyo Dar es Salaam. Jiji lenye majina lukuki ya mtaani ambayo bado yanaondelea kuibuka kila siku kutoka na matukio kadha wa kadha yanayotokea  kila uchwao.
    Ziko hadithi nyingi ndani ya jiji hili ikiwemo ile ya staa mmoja wa soka ambaye inasemekana alishindwa kucheza ughaibuni kisa tu kuna mambo flani ambayo alizoea kuyapata akiwa hapa  nchini hayakuwepo huko alikokwenda.
    Hakuna uhakika wa ndani juu ya hadithi hiyo lakini ukweli unabaki kuwa baada ya miezi michache ya kukaa huko nyota huyo alifunga virago kurejea nchini wakati tayari ilishaanza kutengeneza jina hasa baada ya kuonyesha uwezo mkubwa kwenye michezo kadhaa ya awali.
    Ibrahim Hajib ni mchezaji mwenye kiwango cha kucheza Ulaya

    Nyuma ya hadithi hiyo ipo nyingine inayomuhusu chipukizi wa mchezo huo Ibrahim Hajib anayesukuma ‘gozi’  kwenye kikosi cha mabingwa wa kihistoria  wa afrika mashariki na kati Simba Sports Club.
    Tangu amejuishwa kwenye kikosi cha Simba Sport mnamo 2014, Ajibu amekuwa mchezaji muhimu akifanikiwa kufunga mabao mengi mazuri na pia  kuwaunganisha (assist)  nyota  wengine anaocheza nao kwenye eneo la ushambuliaji katika timu hiyo.

    Hilo la kufunga linathibitishwa na ushindi wake wa tuzo ya mchezaji aliyefunga bao bora  msimu uliopita, akiweka mpira kimiani mara baada ya kukusanya ‘kijiji’ kwenye mchezo wa timu yake dhidi ya  wageni Mgambo JKT ya Tanga kwenye uwanja wa Taifa.
    Vijiweni, kumekuwa na mabishano makali kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka juu ya uwezo wa kijana huyu fundi wa mpira,wengine wakidriki kumtupia lawama kwa kile wanachokiona kuwa licha ya uwezo mkubwa Hajibu anaudharau mpira wa miguu.
    “Ni mchezaji mzuri mwenye kipaji, siku akiacha mambo ya kitoto na kuudharau mpira anaweza kuifanya dunia ikaimba jina lake” hii ni nukuu kutoka ‘posti’ ya mmoja wa wachezaji nyota wa timu ya Yanga kwenye mtandao wa ‘twitter’ akimzungumzia Hajib siku chache zilizopita.
    Japo kuna watu ambao wanaweza kupinga hasa kutokana na mapenzi yao lakini kwa namna moja ama nyingine ukitizama kwa makini na kuzungumza kama mwanamichezo huwezi kuwa mbali na wadau hao wa soka au mawazo ya mchezaji huyo wa Yanga (kwenye nukuu).
    Hajibu ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa uwanjani, anapokuwa na mpira huna shaka kwa njisi atakavyoucheza kwa maana ya kutoa pasi, kupiga krosi au chenga pia kufunga pale anakuwa kwenye nafasi,uwezo mzuri wa kupiga mipira ya adhabu ndiyo mambo yanayomfanya kuwa mchezaji machachari na hatari.
    Wakati  Taifa stars ikipokea kichapo kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe, jijini Harare, mmoja wa wachambuzi wa soka kwenye kituo cha runinga nchini alisikika akimlaumu kocha Mkwasa kwa kuacha kumpa nafasi kijana huyu,akimini ingekuwa njia sahihi ya kumkomaza Hajibu kisoka.
    Ziko lawama nyingi kutoka kwa baadhi ya walimu ambao wamepata nafasi ya kufanya naye kazi wengi wakimlaumu kwa uzembe wa mazoezi, kama alivyothibitisha kocha wa  Polisi Morogoro (jina kapuni) ambaye alimpokea Ajibu  kwa  mkopo akitokea  Simba B mnamo 2012/13.
    Ni wazi unaweza kumaliza kurasa nzima ya gazeti kumuelezea au kudadavua uwezo wa kijana huyu lakini hakuna ubishi kuwa yeye mwenyewe anapashwa kuamka na kuliona hili ikiwa tu anataka kutengeza maisha na heshima nzuri kwake na nchi yake siku za usoni.
    Yapo maswali mengi yasiyo na majibu,ni yeye hataki mafanikio.? au watu wanaomzunguka wameshindwa kumfumbua macho?.. Kipaji alichonacho Hajibu si cha kupigana vikumbo kwenye mashindano  ya ndondo huko vichochoroni, ni kipaji ambacho kinafaa kugombaniwa na makampuni makubwa  kibishara.
    Ili kuyafikia mafanikio Ajibu anapaswa kukubali kuwa mpira bado unamdai vitu vingi,kwa maana kuwa mpaka sasa bado hajafanya lolote kubwa kulingana na kipaji alichonacho,anapaswa kujua kuwa umri alionao sasa ndiyo sahihi katika kuitafuta heshima yake duniani.
    Jambo muhimu ni kutambua kasoro alizonazo na kuzifanyia kazi Cristiano Ronaldo anaendelea kuwa mchezaji mwenye mafanikio zaidi duniani kwa sasa hili linaletwa na juhudi zake katika kufanya mazoezi na  kuuheshimu mchezo wa soka, hili ndilo analotakiwa kufanya Hajibu.
    Hawezi kuwa meneja wa bank, hawezi kuwa daktari bingwa lakini anaweza kuwa mkurugenzi wa kampuni moja kubwa na kuajiri watu wengi kupitia kipaji chake, huu ndiyo wakati anapaswa kufumbua macho na kulia  machozi anapoziona picha za Hotel Pestana CR7 zinazomilikiwa na nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
    Kuna mengi ya kufanya kufika huko, Hajibu anapaswa kujituma kuongeza jitihada, na kuwa na kiu ya mafanikio,hakuna namna nyingine kwenye hili ndiyo maana wajuzi wa mambo husema, soka halina njia fupi,anapaswa kuvaa miwani na kuiona jezi yake ulaya kabla jua halijazama.
    Kwenye moja ya nukuu zake nyota wa zamani wa Real Madrid, Mahamadou Diara, aliwahi kusema, huwezi kuwa mwanasoka mwenye mafanikio bila kujituma,kuishi kwenye mapungufu yako ukiitafuta thamani ya kipaji chako, hakika alikuwa sahihi.
    Hajib vaa miwani uione jezi yako Ulaya kabla jua halijazama.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAJIB VAA MIWANI UIONE JEZI YAKO ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top