• HABARI MPYA

    Monday, December 05, 2016

    "HAJIB, MKUDE BADO WAPO WAPO SANA SIMBA"

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imesema haina matatizo na wachezaji wake, kiungo Jonas Mkude na mshambuliaji Ibrahim Hajib juu ya kusaini mikataba mipya.
    Wawili hao wanamaliza mikataba yao na kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na uongozi wa klabu juu ya kusaini mikataba mipya.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Sunday Manara amesema kwamba wachezaji hao wamekuwa wakihudhuria mazoezi kila siku tangu maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Ibrahim Hajib akipasua katikati ya wachezaji wa Azam FC katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu 
    “Tupo nao (Mkude na Hajib) tangu Jumatano na hawajawahi kukosekana hata siku moja mazoezini. Sisi wenyewe tunashangaa hizo taarifa za kwamba wamegoma”amesema Manara.
    Aidha, Manara alisema kwamba kikosi kizima cha Simba SC kinaondoka leo Dar es Salaam kwenda Morogoro kuweka kambi ya kujiandaa na mzunguko wa Ligi Kuu.
    Alisema wachezaji wote wataondoka leo kwenda Morogoro wakiwemo wale ambao wapo kwenye mazungumzo ya mikataba mipya na kwamba masuala yao yatamalizwa wakiwa kambini.
    “Wanakwenda wote. Hata hawa ambao wapo mbioni kusaini mikataba mipya wanakwenda pia. Mambo yao yatakwenda kumaliziwa huko huko. Hapa kikubwa ni maandalizi,”amesema.
    Wachezaji ambao hadi jana walikuwa hawajaripoti mazoezini ni mabeki wote, Emmanuel Semwanza, Malika Ndeule na Mganda, Juuko Murshid, ambaye ana ruhusa maalum.
    Wachezaji wanaotarajiwa kuondoka leo kwenda kambini Morogoro ni makipa; Vincent Angban, Peter Manyika na Dennis Richard, mabeki; Hamad Juma, Janvier Bokungu, Abdi Banda, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga na Method Mwanjali.
    Viungo ni Awadh Juma, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Mussa Ndusha, Muzamil Yassin, Jamal Mnyate, Shizza Kichuya na washambuliaji Frederick Blagnon, Laudit Mavugo, Ame Ally na Ibrahim Hajib, Hajji Ugando.
    Simba ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika nafasi ya kwanza kwa pointi zake 35, mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: "HAJIB, MKUDE BADO WAPO WAPO SANA SIMBA" Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top