• HABARI MPYA

  Saturday, December 17, 2016

  FARID MUSSA ATAKIWA HISPANIA DESEMBA 27

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WINGA chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Farid Malik Mussa anatakiwa kuwa amefika Hispania Desemba 27, mwaka huu tayari kuanza kuichezea klabu ya CD Tenerrife ya Daraja la Kwanza, maarufu kama Segunda B.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online jana, Farid anayekwenda klabu hiyo kwa mkopo kutoka Azam FC, alisema kwamba kwa sasa anasubiri kutumiwa tiketi tu na Tenerrife.
  “Mambo sasa yamekamilika kila kitu. Ubalozi wa Hispania hapa umenipa vibali vyote vya kwenda kufanya kazi kule, nachosubiri kwa sasa ni tiketi kutumwa na Tenerrife ili niende na viza yangu inaonyesha natakiwa niwe nimekwishafika kule hadi Desemba 27,”alisema Farid.
  Farid Mussa anatakiwa kufika Hispania Desemba 27, mwaka huu tayari kuanza kuichezea CD Tenerrife 

  Farid ambaye hajacheza mechi yoyote msimu huu kwa kuchelewa kupata kibali, alisema kwamba kipindi chote amekuwa akifanya mazoezi na Azam FC kujiweka fiti.
  Azam FC imemtoa kwa mkopo Farid kwenda CD Tenerife kwa makubaliano maalum. Na hiyo ilifuatia Farid kufuzu majaribio katika klabu hiyo katikati ya mwaka alipokwenda na Mkurugenzi wa klabu yake, Yussuf Bakhresa.
  Farid alitua Hispania Aprili 21 baada ya kuichezea Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance mjini Tunis, Tunisia ikifungwa 3-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
  Na ilimchukuwa wiki moja tu Farid kuwakuna kwa kipaji chake makocha wa Tenerife na kutaka kumnunua, lakini Azam ikakataa na kuamua kumtoa kwa mkopo.
  Azam FC haijamsajili Farid katika kikosi chake cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu kwa kuwa imemtoa kwa mkopo Tenerife ambayo tayari imemuombea hadi Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: FARID MUSSA ATAKIWA HISPANIA DESEMBA 27 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top