• HABARI MPYA

  Friday, November 04, 2016

  ZANZIBAR WAHOFIA KUZIKOSA SIMBA NA YANGA KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Salum Vuai, ZANZIBAR
  HUKU ikiwa imebakia miezi isiyozidi miwili kabla kuanza kwa sherehe za kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, huenda klabu vigogo za Tanzania Bara zisishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.
  Ikumbukwe kuwa, imekuwa ni mazoea kwa mashindano hayo yenye mvuto wa pekee Afrika Mashariki, kushirikisha klabu kongwe za Yanga SC na Simba SC pamoja na Azam FC za Dar es Salaam.
  Aidha, mara kadhaa klabu nyengine za Bara zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kama vile Mtibwa Sugar na Coastal Union zimekuwa zikijumuishwa kuyaongezea msisimko mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka hapa Zanzibar. 
  Wasiwasi wa kutokuwemo kwa klabu hizo kwenye michuano ya mwakani, umeibuka kutokana na kalenda ya Ligi Kuu Bara kutoonyesha kusita kwa ligi hiyo kupisha ngarambe hizo.
  Kwa kawaida, mashindano hayo huanza mwishoni kabisa mwa mwezi wa Disemba au mapema Januari kila mwaka na kumalizika ama Januari 12 au 13, baada ya kilele cha maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
  Hata hivyo, wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiwa limeainisha katika ratiba ya Ligi Kuu msimu huu tarehe ambazo ligi hiyo itasita kupisha baadhi ya michuano ya kimataifa, haioneshi kusimama kwake wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi.
  Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Januari 1, 2017, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Yanga SC, watashuka dimbani kuivaa African Lyon.
  Aidha, Januari 7, 2017 wakati michuano ya Mapinduzi huwa inaingia hatua ya nusu fainali, kutakuwa na mechi saba za Ligi Kuu hiyo ya Bara, ambapo tarehe 8 Januari, kutachezwa mechi moja, Yanga SC, Simba SC na Azam FC zikicheza kwa siku tafauti.
  Wakati Januari 7 Yanga itakuwa ikirudiana na Ndanda FC jijini Dar es Salaam na Azam FC wakiwa wenyeji wa Tanzania Prisons, Januari 8, wekundu wa Msimbazi Simba SC watakuwa ugenini mkoa wa Pwani kumenyana na Ruvu Shooting.
  Wakati TFF ikiiweka kando michuano ya Kombe la Mapinduzi, ligi hiyo itasimama kati ya Novemba 7 na 15 mwaka huu kutoa nafasi ya kuchezwa mechi za kimataifa zilizomo kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
  Aidha, ratiba hiyo inaonesha kuwa Novemba 19 na 20, itakuwa wiki ya mechi za Kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo hata hivyo, hakuna timu ya Tanzania inayoshiriki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ZANZIBAR WAHOFIA KUZIKOSA SIMBA NA YANGA KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top