• HABARI MPYA

    Saturday, November 19, 2016

    YANGA YAFIKIRIA KUTOSAJILI WAGENI DIRISHA DOGO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KUNA uwezekano usajili wa dirisha dogo ndani ya klabu ya Yanga usihusu mchezaji wa kigeni, badala yake wanaweza kusajiliwa wachezaji wazawa wasiozidi wawili.
    Habari kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba klabu imeamua kuwapa nafasi nyingine hadi mwishoni mwa msimu wachezaji wake wa kigeni - maana yake kiungo Mzambia Meshack Chaila na mshambuliaji Mkenya Jesse Were wanaotajwa kutakiwa wanaweza wasisajiliwe. 
    Chaila na Were wote walikuwa wachezaji tegemeo wa kocha mpya wa Yanga, George Lwandamina katika kikosi cha Zesco United kilichofika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu kabla ya kutolewa na Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini iliyofanikiwa kutwaa taji hilo.
    Meshack Chaila akkimtoka Amr Gamal wa Al Ahly (kulia) katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi

    Lakini habari za uhakika zaidi zinasema kwamba, Yanga inataka kusajili viungo wawili wazawa katika kipindi hiki cha dirisha dogo ili kujiimarisha kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
    Inaelezwa kwamba Yanga inataka kusajili kiungo mkabaji na kiungo mchezeshaji, hayo yakiwa mapendekezo ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye sasa anakuwa Mkurugenzi wa Ufundi, akimpisha Mzambia, George Lwandamina.  
    Na wachezaji ambao inadaiwa wapo kwenye rada za Yanga kwa ajili ya nafasi hizo wote ni kutoka Mbeya City, Kenny Ally kiungo mkabaji na Raphael Daudi kiungo mchezeshaji.
    Yanga imeona kama kusajili mchezaji wa kigeni, bora isibiri hadi mwakani kama timu itafuzu 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho. Lakini uongozi unaweza kuchukua hatua yoyote tofauti kulingana na matakwa ya kocha mpya, Lwandamina.
    Kwa sasa wachezaji wa Yanga wapo likizo hadi Novemba 28 na Lwandamina anaandaa programu yake ya mazoezi kwa maandalizi ya mzunguko wa pili.
    Yanga imepania kurudia mafanikio yake ya msimu uliopita kushinda mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
    Yanga pia ilifika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria, baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAFIKIRIA KUTOSAJILI WAGENI DIRISHA DOGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top