• HABARI MPYA

    Wednesday, November 16, 2016

    WAWA ATAJA SABABU ZA KUREJEA EL MERREIKH

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI Serges Pascal Wawa amesema kwamba amechagua kurudi El Merreikh kwa sababu ni sehemu salama kwa soka yake.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwa simu kutoka Nairobi, Kenya, Wawa alisema kwamba Merreikh ni timu kubwa Afrika na Khartoum ni kama nyumbani.
    “Ninarudi Merreikh. Kule ni nyumbani, kumbuka nilikuja hapa nikitoka Merreikh na sasa baada ya kumaliza Mkataba wangu narudi Sudan,”amesema.
    Wawa aliyejiunga na Azam FC mwaka 2014 amesema kwamba Ligi ya Sudan ni kubwa kuliko ya Tanzania na ina ushindani zaidi.
    Serge Wawa Pascal (katikati) akisaini mkataba wa El Merreikh jana mjini Nairobi
    “Na Merreikh inashiriki mashindano ya Afrika inafika mbali, nimekumbuka kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa. Nafasi hii naweza kuipata nikiwa Merreikh,”amesema.
    Wawa mwenye umri wa miaka 30 sasa, kisoka aliibukia katika akademi ya ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast mwaka 2003.
    Na akiwa na umri wa miaka 19 tu mwaka 2009, Wawa alikwenda kufanya majaribio FC Lorient ya Ufaransa, ambako kwa bahati mbaya hakufanikiwa.
    Desemba mwaka 2010 alijiunga na vigogo wa Sudan, El-Merreikh kwa mkataba wa miaka mitatu kabla ya Novemba 2014 kuhamia Azam FC ya Tanzania.
    Baada ya takriban misimu miwili ya kuwa na Azam FC akishinda taji la Ligi Kuu na Ngao ya Jamii, Wawa aliyeichezea Ivory Coast katika Olimpiki mwaka 2008 anarejea Sudan.
    Amekutana na viongozi wa Merreikh mjini Nairobi jana na kusaini Mkataba wa miaka miwili kurejea Sudan. Leo alikuwa anashughulikia visa ya kwenda huko na familia yake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAWA ATAJA SABABU ZA KUREJEA EL MERREIKH Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top