• HABARI MPYA

  Tuesday, November 01, 2016

  WATANO WAKAMATWA KWA MAUWAJI YA MASHALI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WATUHUMIWA watano wa mauaji ya bondia Thomas Fabian Mashali maarufu ‘Simba Asiyefungika’ wamekamatwa leo Kimara mjini Dar es Salaama.
  Kaka wa marehemu, Emmenuel Mashali ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo kwamba wamefanikiwa kuwasaidia Polisi kuwatia nguvuni watuhumiwa watano wa mauaji wa ndugu yao.
  “Tupo na Polisi huku Kimara tunawasaidia kuwapata watuhumiwa. Tumefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano, na tumewaleta kituo kidogo cha Polisi Kimara. Lakini watapelekwa kituo kikubwa cha huku (Mbezi). Baada ya hapo ndio watapelewa mahakamani. Wawili tumewakamata KImara Bonyokwa na watatu KImara Salanga,”amesema Emmanuel Mashali.
  Bondia Thomas Mashali (kushoto) akiinuliwa mkono dhidi ya Sajjad Mehrabi wa Iran Mei 14 mwaka huu baada ya ushindi wa pointi Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam na kutwaa ubingwa wa dunia wa UBO uzito wa Super Middle

  Hata hivyo, alipoulizwa Kamanda wa Polisi wa Kanda maalum ya Kinondoni, Dar es Salaam, Susan Kaganda amesema hawawezi kusema chochote kwa sasa hadi hapo watakapokamilisha uchunguzi wao.
  Bingwa wa zamani wa mataji mbalimbali, Mashali alifariki dunia usiku wa kuamkia jana baada ya ugomvi uliotokea Kimara Bonyokwa dhidi ya watu wasiojulikana.
  Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa viwanja vya Leaders Club kuanzia Saa 5:00 hadi Saa 9:30 mchana kesho kabla ya mazishi yatakayofanyika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
  Hadi anakutwa na umauti, Mashali alikuwa amepigana jumla ya mapambano 26 ya ngumi za kulipwa akishinda 19, kushindwa matano, sare moja na moja lilifutwa ulingoni.
  Enzi za uhai wake, Mashali alikuwa mkali kweli ulingoni akishinda mataji tofauti kuanzia la Afrika Mashariki na KatiOktoba 14, mwaka 2012 kwa kumpiga Med Sebyala wa Uganda kwa pointi ukumbi wa Friends Corner, Dar es Salaam.
  Akalitetea taji hilo kwa kumpiga Mkenya Bernard Mackoliech Januari 12, mwaka 2013, ukumbi wa Friends Corner, hivyo kupata nafasi ya kwenda kuwania taji la IBF Afrika, ambalo hata hivyo alilikosa kwa kupigwa na Mtanzania mwenzake, Francis Cheka Mei 1, mwaka 2013 kwa Knockout (KO) raundi ya saba ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
  Mashali akashindwa pia kutwaa taji la Mabara la UB Novemba 16, mwaka 2013 baada ya kupigwa na Mrusi Arif Magomedov ukumbi wa Ivanhoe Country Club, mjini Podolsk, Urusi kwa KO raundi ya saba.
  Akasahihisha makosa yake na kufanikiwa kutwaa taji la UBO Afrika kwa kumpiga kwa pointi Mtanzania mwenzake, Japhet Kaseba Machi 29, mwaka 2014 ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
  Akatetea taji hilo kwa kumpiga Alibaba Ramadhani Oktoba 5, mwaka 2014 kwa KO raundi ya tisa pambano la raundi 12 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, kabla ya kwenda kupigwa na Mrusi Apti Ustarkhanov kwa KO raundi ya pili ukumbi wa Colosseum Sport Hall, mjini Grozny, Urusi Machi 5, 2016.
  Mashali akarudisha heshima Mei 14 mwaka huu kwa kumpiga Sajjad Mehrabi wa Iran kwa pointi Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa dunia wa UBO uzito wa Super Middle.
  Julai 9, mwaka huu alishindwa kutwaa taji la WBO Oriental uzito huo huo wa Super Middle baada ya kupigwa na Mchina Zulpikar Maimaitiali kwa KO raundi ya sita ukumbi wa Multi-Functional Hall, Water Cube mjini Beijing, China.
  Akaweka kumbumbu ya kushinda pambano la mwisho kabla ya kifo chake, kwa kumpiga Shaaban Kaoneka kwa pointi ukumbi wa Chee Kwa Chee Pub, Bagamoyo mkoani Pwani Septemba 12, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WATANO WAKAMATWA KWA MAUWAJI YA MASHALI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top