• HABARI MPYA

  Wednesday, November 09, 2016

  VIONGOZI TFF WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUOMBA RUSHWA SH MILIONI 25

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSAIDIZI wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Juma Matandika na Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Martin Chacha leo wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh. Milioni 25.
  Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi aliyembangiwa kusikiliza kesi hiyo katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
  Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru, Leonard Swai akisaidiana na Odessa Horombe.
  Juma Matandika (kulia) amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh. Milioni 25

  Swai alidai kuwa alidai  Februari 4 mwaka huu  Matandika na Chacha wote kwa pamoja wanadaiwa  kuomba rushwa kinyume cha sheria ya kuzuia rushwa.
  Ilidaiwa kuwa Februali 4 mwaka huu, makao makuu ya TFF washtakiwa wakiwa waajiriwa wa shirikisho hilo, walishawishi na  kuomba rushwa ya Sh. milioni 25 kutoka kwa Salum Kulunge na Constantine Morandi.
  Upande wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa Kulunge na Morandi ni maafisa kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita na Klabu ya Mpira wa Miguu Geita na kwamba  washtakiwa waliomba rushwa kama kishawishi kwa TFF na Idara ya Uhamiaji Tanzania kutoa uamuzi wa dhidi ya Klabu ya Mpira wa Miguu Polisi Tabora ili kuisadia Klabu ya Geita kupanda katika Ligi Kuu Tanzania.
  Washtakiwa walikana mashtaka hayo na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi umekamilika.
  Swai aliomba mahakama ya kupanga tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali.
  Hata hivyo, mahakama ilikubali kuwapa dhamana washtakiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili, wenye barua na vitambulisho watakaosaini dhamana ya maandishi ya Sh. milioni tano kila mmoja.
  Washtakiwa wametimiza masharti ya dhamana wako ne hadi Novemba 30 mwaka huu kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
  Kamati ya Nidhamu ya TFF chini ya Makamu Mwenyekiti, Wakili Jerome Msemwa, ilitoa uamuzi kuzishusha daraja timu nne; Geita Gold, Polisi Tabora, Oljoro JKT na Kanembwa JKT kutokana na kile ilichoeleza kuwa kubaini upangaji wa matokeo wa mechi zake za mwisho za Kundi C za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu uliopita.
  Wakili Msemwa alisema timu hizo za mikoa ya Geita, Tabora, Arusha na Kigoma zilikutwa na hatia ya upangaji wa matokeo na kupewa adhabu ya kushushwa daraja mpaka Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu huu.
  Kutokana na kushika mkia katika Kundi C, JKT Kanembwa FC ilishushwa mpaka kwenye ngazi ya Ligi ya Mkoa (RCL).
  Baada ya hukumu hizo za kisoka, baadhi ya viongozi wa timu hizo zilizoporomoshwa daraja, waliibuka na kudai kuwa kabla ya hukumu kutoka, walikuwa wakipigiwa simu na baadhi ya watendaji wa TFF wakiwaomba rushwa ilitimu zao zisishushwe daraja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: VIONGOZI TFF WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUOMBA RUSHWA SH MILIONI 25 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top