• HABARI MPYA

  Thursday, November 03, 2016

  SIMBA WAREJEA LEO KWA ‘PIPA’ MOJA KWA MOJA KAMBINI, JUMAPILI NA LYON

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC inatarajiwa kurejea leo jioni mjini Dar es Salaam kwa ndege na moja kwa moja kuingia kambini, Ndege Beach kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Simba itawasili jioni ya leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ikitokea Mwanza ambako itapita kuunganisha usafiri wa anga baada kusafiri kwa barabara kutoka Shinyanga. 
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kwamba mara kikosi kitakapowasili kitakwenda moja kwa moja kambini Ndege Beach, Mbweni, nje kidogo ya Dar es Salaam.
  Simba SC inarejea leo jioni mjini Dar es Salaam kwa ndege na moja kwa moja kuingia kambini, Ndege Beach kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara

  Manara alisema kikosi kitafanya mazoezi ya siku moja kesho kabla ya kuingia kwenye mchezo wake mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya African Lyon Jumapili Dar es Salaam.
  Ikumbukwe jana Simba imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya timu ngumu msimu huu, Stand United ya Shinyanga.
  Ushindi huo, unaifanya Simba SC ifikishe pointi 35 baada ya kucheza mechi 13, wakati Stand inabaki na pointi zake 22 za mechi 14. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa, Shomary Lawi wa Kigoma aliyesaidiwa na Mirambo Tshikungu na Robert Ruhemeja, Simba walipata bao lao mapema kipindi cha kwanza.
  Bao hilo lilifungwa na winga machachari wa Wekundu hao wa Msimbazi, Shizza Ramadhani Kichuya kwa penalti dakika ya 33 baada ya mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo kuangushwa na beki Adeyum Ahmed kwenye boksi.
  Baaada ya bao hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini ni Simba SC waliokuwa waking’ara uwanjani.
  Mapema dakika ya nane, Kichuya aliunganishia nje kwa kichwa krosi ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kabla ya Nahodha wa Stand United, Jacob Massawe kupiga juu kufuatia krosi ya Frank Hamisi.
  Kipindi cha pili, mchezo uliendelea kuwa wa mashambulizi ya pande zote mbili, lakini Simba inayofundishwa na Mcameroon, Joseph Marius Omog ilifanikiwa kuulinda ushindi wake.
  Na Simba SC ilikaribia kupata bao la pili dakika ya 65 kama si kiungo Mohamed ‘Mo’ Ibrahim kupiga juu ya lango kufuatia pasi nzuri ya Kichuya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA WAREJEA LEO KWA ‘PIPA’ MOJA KWA MOJA KAMBINI, JUMAPILI NA LYON Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top