• HABARI MPYA

    Sunday, November 06, 2016

    SIMBA SC 'WAVUTWA MKIA' SHAMBA LA BIBI, DOGO LA JANGWANI LACHINJA MNYAMA

    Na Princess Asia, DAR ES WALAAM
    BAO la dakika ya 89 la kiungo wa zamani wa Yanga, Abdallah Mguhi 'Messi' limetosha kuipa African Lyon ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Mguhi 'Messi' aliyeibukia Yanga B mwaka 2013 na kucheza kwa muda mfupi Yanga A enzi za kocha Mholanzi Ernie Brandts, alifunga bao hilo leo pekee dakika ya 89 akimalizia krosi ya Miraj Adam kutoka kulia.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na Ahmada Simba wa Kagera, aliyesaidiwa na Soud Lilla na Frank komba wote wa Dar es Salaam, dakika 45 za kipindi cha kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu.
    Wachezaji wa Simba wakiwa hawaamini macho yao baada ya Lyon kukosa bao la wazi kipindi cha kwanza

    Simba hawakuwa katika ubora leo kutokana na mfumo uliotumiwa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog akianzisha viungo watano na mshambuliaji mmoja tu, Mrundi Laudit Mavugo ambaye alishindwa kufurukuta.
    Beki Mkongo Janvier Besala Bokungu alikaribia kuifungia Simba dakika ya 19 baada ya kupiga shuti, ambalo kipa Mcameroon wa Lyon, Rostand Youthe alidaka.
    Beki Miraj Adam alikaribia kuiadhibu timu yake ya zamani dakika ya 39 baada ya kupiga shuti la mpira wa adhabu lililogonga mwamba wa lango na kutoka nje.
    Kipindi cha pili Omog alianza kwa kuiongezea makali safu ya ushambuliaji akimtoa kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na kumuingiza mshambuliaji Ibrahim Hajib.
    Angalau kidogo Simba SC ikaanza kulitia misukosuko lango la African Lyon, ambayo sehemu kubwa ya kipindi cha pili ilicheza mchezo wa kujihami ikitumia mashambulizi ya kushitukiza.
    Kwa matokeo hayo, SImba inabaki na pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 14 ingawainaendelea kuongoza Ligi Kuu mbele ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 30 za mechi 14 pia.
    Kikosi cha African Lyon kilikuwa; Rostand Youthe, Miraj Suleiman, Baraka Jaffar, Hamad Waziri, Isihaka Hassan, Omar Salum, Awadh Juma, Khalfan Twenye/Rehani Kibingu dk88, Hamad Manzi/Amani Peter dk63, Abdallah Mguhi ‘Messi’ na Omar Abdallah. 
    Simba SC; Vincent Angban, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shizza Kichuya, Muzamil Yassin, Mohamed ‘Mo’ Ibrahim/Ibrahim Hajib dk50, Laudit Mavugo/Said Ndemla dk81 na Mwinyi Kazimoto/Jamal Mnyate dk76. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC 'WAVUTWA MKIA' SHAMBA LA BIBI, DOGO LA JANGWANI LACHINJA MNYAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top