• HABARI MPYA

  Tuesday, November 15, 2016

  SIMBA SC: HATUNA TATIZO LA MISHAHARA, WACHEZAJI WOTE WANALIPWA KWA WAKATI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa Simba SC umesema kwamba wachezaji wa klabu hiyo wanalipwa mishahara yao ndani ya muda na hakuna mchezaji hata mmoja anayecheleweshewa au kutolipwa mshahara wake.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana, Katibu Mkuu wa Simba SC, Patrick Kahemele alisema kwamba wanastaajabishwa na taarifa za tatizo la mishahara katika klabu yao wakati hazipo.
  “Awali tulizipuuza hizi taarifa, maana si kila taarifa ni za kukanusha, nyingine ni za kupuuza tu, lakini naona watu wanaanza kuziamini. Napenda niseme hakuna tatizo la mishahara Simba SC, wachezaji wote wanalipwa stahiki zao kwa wakati,”alisema Kahemele.
  Pamoja na hayo, Katibu huyo wa Simba SC alisema kwamba wachezaji wa klabu hiyo wamepewa mapumziko ya wiki mbili baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kukiwa hakuna mtu anayedai.
  “Kila taasisi ina utaratibu wake wa kulipa mishahara. Na sisi kama Simba SC tuna utaratibu wetu. Ndani ya utaratibu wetu hakuna anayekosa haki yake na wote wanalipwa kwa wakati kulingana na utaratibu tuliojiwekea,”alisema.
  Kufuatia Simba SC kufungwa mechi mbili mfululizo za mwisho za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 1-0 na African Lyon Dar es Salaam na 2-1 na Prisons Mbeya baada ya mwanzo mzuri wa kucheza 13 bila kupoteza, ikishinda 11 na sare mbili, zikaibuka taarifa za wachezaji kutolipwa mishahara kwa miezi mitatu.
  Taarifa hizo za kwenye magazeti ya mwishoni mwa wiki zimewakera baadhi ya wanachama na wapenzi wa Simba, wakiamini ndizo zilichangia timu kufungwa na Lyon na Prisons. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC: HATUNA TATIZO LA MISHAHARA, WACHEZAJI WOTE WANALIPWA KWA WAKATI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top