• HABARI MPYA

  Monday, November 07, 2016

  SHEIKH SAID WA AZAM HATUNAYE; “INNA LYLLAH WAINNA ILAYH RAJIUUN”

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Azam FC, Sheikh Said Muhammad Abeid amefariki dunia jioni ya leo katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
  Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jioni hii kwamba Sheikh Said amefariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo.
  Sheikh Said Muhammad amefariki dunia jioni ya leo katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam

  “Hakuwa anaumwa, ni leo hali yake ilibadilika ghafla akapelekwa hospitali na familia yake, ambako ndiko umauti umemfika. Siwezi kusema zaidi kwa sasa, acha kwanza nifike hospitali nipate taarifa zaidi,”amesema Kawemba.

  Mbali na kuwa Mwenyekiti wa Azam FC, Sheikh Said Muhammad pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu.   
  Taarifa za awali zinasema Sheikh Said Muhammad atazikwa kesho makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam Saa 10:00 baada ya mwili wake kusaliwa msikiti wa Maamur, Upanga.
  Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Nassor Idrisa 'Father' amesema kwamba Sheikh Said Mohamed, atakumbukwa kama mmoja wa nguzo muhimu kwenye mafanikio ya klabu ya Azam FC tangu kuanzishwa kwake miaka takribani nane iliyopita.
  "Chini ya uongozi wake kama mwenyekiti wa Azam FC, aliiongoza klabu hii kunyakuwa mataji mbalimbali makubwa na kwa mafanikio, ikiwemo taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Mapinduzi mara mbili pamoja na Ngao ya Jamii,".
  "Si hivyo tu, mchango wake Mzee Said Mohamed hauku-ishia nyumbani kwake Azam FC tu, bali hata kwenye familia ya soka la Tanzania kwa ujumla wake ambapo hadi umauti unamkuta alikuwa ni makamu mwenyekiti wa bodi ya ligi kuu Tanzania bara na mjumbe wa kamati mbalimbali za shirikisho la soka Tanzania, TFF,".
  "Sisi Azam FC, tutamkumbuka Mzee Said Mohamed kwa ucheshi wake, ukarimu na uchapakazi wake kwa ujumla," alisema Father.
  Sheikh Said alizaliwa Machi 20 mwaka 1940 visiwani Zanzibar na anatarajiwa kuzikwa kesho katika makaburi ya Kisutu baada ya sala ya Alasiri, kufuatia mwili wake kutasaliwa msikiti wa Maamour, Upanga.
  Mwenyezi Mungu ailaze roho yake Said Mohamed Abeid mahali pema peponi, Amiin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SHEIKH SAID WA AZAM HATUNAYE; “INNA LYLLAH WAINNA ILAYH RAJIUUN” Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top