• HABARI MPYA

  Saturday, November 12, 2016

  PLUIJM: YANGA IPO MKAO WA KUBEBA TAJI LA TATU MFULULIZO LA LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BAADA ya kumaliza vizuri mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm amesema kwamba anawania taji la tatu mfululizo la ubingwa wa michuano hiyo.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana, Pluijm alisema kwamba ushindi wa juzi unaiweka katika nafasi nzuri Yanga kuelekea kutwaa taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu.
  “Ninachotaka kukuambia ni kwamba bado tupo kwenye mbio za taji la tatu mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,”alisema Mholanzi huyo jana.
  Na alipoulizwa kuhusu Ligi Kuu ya msimu huu kulinganisha na ya msimu uliopita, Pluijm alisema; “Ukweli ni kwamba timu zote zinaimarika hatua kwa hatua. Hii inamaanisha kwamba ushindani unaongezeka katika Ligi kila mwaka,”.  
  Baada ya ushindi wa 2-1 katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam juzi, Yanga inamaliza katika nafasi ya pili kwa pointi zake 33 nyuma ya Simba SC yenye pointi 35 kileleni baada ya mechi 15.
  Sifa zimuendee kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kwa ushindi wa juzi kutokana na kuseti bao la kwanza lililofungwa na winga na Simon Msuva na kufunga bao la pili, wakati bao la Ruvu lilifungwa Abrahman Mussa.
  Lakini kuna uwezekano Pluijm asirejee kwenye benchi la Ufundi la Yanga kutokana na klabu hiyo kudaiwa kuingai mkataba wa siri na kocha Mzambia, George Lwandamina atakayeanza kazi mzunguko wa pili wa Ligi Kuu. 
  Hadi sasa, katika awamu mbili ambazo Pluijm ameiongoza Yanga tangu mwaka 2014, imecheza jumla ya mechi 128, ikishinda 80, kufungwa 23 na sare 25.
  Mwaka 2014 aliiongoza Yanga katika mechi 19, akishinda 11, kufungwa mbili na sare sita kabla ya kuondoka kwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo.
  Maximo alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana.  Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm  aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.
  Na kuanzia Januari mwaka jana, Pluijm ameiongoza Yanga katika mechi 109, akishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.
  Tayari Pluijm ameipa Yanga mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Ngao ya Jamii na moja Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PLUIJM: YANGA IPO MKAO WA KUBEBA TAJI LA TATU MFULULIZO LA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top