• HABARI MPYA

    Friday, November 04, 2016

    PLUIJM: SIKUBALI KUWAACHIA UBINGWA SIMBA HADI MIFUPA YOTE ISAGIKE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mholanzi wa Yanga, Hans va der Pluijm amesema kwamba ataendelea kupambana hadi tone la mwisho la damu ili kuhakikisha anatetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Yanga sasa inazidiwa pointi nane na Simba SC wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 35 za mechi 13, baada ya matokeo ya michezo ya juzi. Wakati Simba ilishinda 1-0 dhidi ya Stand United Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Yanga ilifungwa 2-1 na Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.  
    Na akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana kwa simu kutoka Mbeya, Pluijm alisema kwamba; “Sikubali kushindwa hadi mifupa yote isagike. Hiyo ndiyo sera yangu,” alisema baada ya kuulizwa kama kama bado ana ndoto za kutetea ubingwa.
    Hans van der Pluijm amesema hakubali kushindwa hadi mifupa yote isagike 

    Aidha, Pluijm pia alimlalamikia refa Rajab Mrope wa Ruvuma kwamba alilikubali bao la pili la Mbeya City jana baada ya ushauri wa Kamanda wa Polisi Mbeya, Dhahiri Kidavashali.
    Alisema kwamba halikuwa bao halali na refa alikwishalikataa awali, lakini kwa agizo la Kidavashali akalikubali. 
    “Bao la pili lilikuja baada ya mpira wa adhabu tena. Refa aliwarudisha nyuma wachezaji wetu na kuwaambia wasubiri filimbi na wakati huo huo bila filimbi ya refa wakapiga mpira wa adhabu na kufunga ikawa 2-0,”.
    “Wachezaji wetu walilalamikia lile bao na akakubali kwamba Mbeya City lazima warudie kupiga mpira ule. Mengi (vurugu) yakatokea kisha Kamanda wa Polisi Mbeya akawashauri marefa kulikubali lile bao,”alisema Pluijm.
    Lakini Kivadashali amekana tuhuma za Pluijm akisema; “Sikumuamuru refa, nilichokifanya, baada ya mashabiki wa Mbeya City kuanza kutupa mawe uwanjani, niliwaamuru Polisii waende kuwadhibiti na kumlinda refa,”.
    Na Kamanda huyo akasema kwamba anashukuru vijana wake walifanya kazi yao vizuri mchezo ulimalizika salama na kuhusu maamuzi ya marefa yeye hahusiki na hakuingilia.
    Pluijm alisema bao lile lililokuja wakati timu yake inasaka bao la kusawazisha kufuatia Mbeya City kutangulia kwa bao la mapema dakika ya sita, liliwavunja nguvu vijana wake.
    Mholanzi huyo amesema kwamba pamoja na ukweli huo, timu yake jana haikucheza vizuri kwa ujumla.  
    “Tulizungumza sana kabla ya mchezo, na niliwaonya (wachezaji) kuwa makini, hatukuuanza mchezo kwa umakini wa kutosha. Tukafungwa bao dakika ya sita kutokana na mpira wa adahbu baada ya makosa ya kipa Dida (Deo Munishi) ambaye alikuwa hajajipanga vizuri,”.
    “Hii haikuisaidia timu pia kurudi mchezoni, ilikuwa siku mbaya sana kwetu. Hatukucheza mchezo wetu wa pasi,”alisema.
    Yanga jana ilipoteza mechi ya pili katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kufungwa mabao 2-1 na 
    Mbeya City Council FC  Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Kwa matokeo hayo, mabingwa watetezi, Yanga wanabaki na pointi zao 27 za mechi 13 na sasa wanazidiwa pointi nane na mahasimu, Simba SC wenye pointi 35 za mechi 13 pia.
    Mabao ya MCC jana yalifungwa na Hassan Mwasapili dakika ya sita na Nahodha Kenny Ally dakika ya 36, wakati la Yanga lilifungwa na Mzimbabwe, Donald Ngoma dakika ya 45 na ushei.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM: SIKUBALI KUWAACHIA UBINGWA SIMBA HADI MIFUPA YOTE ISAGIKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top