• HABARI MPYA

    Friday, November 04, 2016

    MKWASA ATAJA KIKOSI CHA STARS KUIVAA ZIMBABWE NOVEMBA 13 HARARE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
    KOCHA Mkuu wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars), Charles Boniface Mkwasa leo Novemba 04, 2016 ametaja majina ya nyota 24 watakaounda kikosi ambacho kitasafiri wiki ijayo kwenda Harare, Zimbabwe kucheza na wenyeji kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Novemba 13, mwaka huu.
    Mkwasa maarufu kwa jina la Master amesema wachezaji aliowaita wataingia kambini Novemba 07, 2016 kabla ya kuanza kukiandaa kikosi hicho siku inayofuata ikiwa mara baada ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara ya mwishoni mwa wiki hii ambako itakuwa funga dimba la duru la kwanza la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2016/17.
    Mkwasa ameita wachezaji 24 watakaosafiri wiki ijayo kwenda Harare, Zimbabwe kucheza na wenyeji kwenye mchezo wa kirafiki wa Novemba 13 

    Nyota wa Stars walioitwa na Mkwasa ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga, Said Kipao wa JKT Ruvu na Aishi Manula wa Azam FC.
    Mabeki; Erasto Nyoni, David Mwantika wa Azam FC, Michael Aidan wa JKT Ruvu, Mwinyi Hajji, Vincent Andrew wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba SC na James Josephat wa Prisons.
    Viungo wa kati ni Himid Mao wa Azam FC, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Jonas Mkude na Muzamil Yassin wa Simba SC, wakati viungo wa pembeni ni Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting, Shizza Kichuya, Jamal Mnyate wa Simba SC na Simon Msuva wa Yanga.
    Washambuliaji ni Ibrahim Hajib wa Simba SC, John Bocco wa Azam FC, Elius Maguli wa Oman Club, Thomas Ulimwengu aliyemaliza mkataba wake TP Mazembe ya DRC na kundoka mwezi uliopita, Omar Mponda wa Ndanda FC na Nahodha Mbwana Samatta wa K.R.C Genk ya Ubelgiji.
    Kwa sababu mbalimbali hususani majeruhi, Mkwasa amewaacha wachezaji Shomari Kapombe wa Azam FC, Hassan Kabunda wa Mwadui FC, Juma Abdul na Juma Mahadhi wa Yanga.
    Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika jijini Harare, umeratibiwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo huwa na kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa kwa wanachama wake – Tanzania ni miongoni mwao. Shirikisho la Mpira wa Miguu la Zimbamwe liliomba TFF mchezo huo, nasi mara moja tukakubali.
    Hii ni faida kwa Tanzania kama itashinda mchezo huo kwa maana kuna alama za nyongeza kama inatokea unaifunga timu mwenyeji.
    Matokeo ya mchezo huo, ni sehemu malumu kupima viwango vya ubora na uwezo wa timu za taifa. Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 144 kati ya nchi 205 wanachama wa FIFA zilizopimwa ubora. Zimbambwe yenyewe inashika nafasi ya 110.
    Argentina inaongoza ikifuatiwa na Ubelgiji anakocheza Mbwana Samatta – nyota wa kimataifa wa Tanzania. Samatta anacheza klabu ya K.R.C Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji. Timu nyingine bora kimataifa ni Chile, Colombia na Ujerumani.
    Katika Bara la Afrika, Ivory Coast ambayo ni ya 31 kwa ubora duniani ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Senegal (32), Algeria (35), Tunisia (38) na Ghana (45).
    Wachezaji wa Zimbabwe watakaochuana na Tanzania ni makipa: Tatenda Mukuruva (Dynamos) na Donovan Bernard (How Mine).
    Mabeki: Godknows Murwira (Dynamos), Hardlife Zvirekwi (CAPS United), Ronald Pfumbidzai (CAPS United), Honest Moyo (Highlanders), Lawrence Mhlanga (Chicken Inn) na Teenage Hadebe (Chicken Inn).
    Viungo: Tendai Ndlovu (Highlanders), Farai Madhanhanga (Harare City), Jameson Mukombwe (Chapungu), Tafadzwa Kutinyu (Chicken Inn), Ronald Chitiyo (Harare City), Talent Chawapihwa (ZPC Kariba) na Malvern Gaki (Triangle).
    Washambuliaji: Pritchard Mpelele (Hwange), Gift Mbweti (Hwange), Leonard Tsipa (CAPS United), Rodreck Mutuma (Dynamos) na William Manondo (Harare City).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKWASA ATAJA KIKOSI CHA STARS KUIVAA ZIMBABWE NOVEMBA 13 HARARE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top