• HABARI MPYA

  Friday, November 11, 2016

  MALINZI AHUZUNISHWA NA MSIBA WA HAFIDH ALI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Dimani Fumba, Zanzibar, Mheshimiwa Hafidh Tahir Ali aliyefariki dunia kwenye Hospitali Kuu ya Dodoma usiku wa kuamkia leo Novemba 11, 2016.
  TFF ilijulishwa kifo cha Mheshimiwa Hafidh na Mbunge wa Jimbo jipya la Ulyankulu, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, John Kadutu ambaye alisema leo walikuwa na programu ya kusafiri kwenda Tabora kushiriki mazishi ya Mbunge wa zamani wa Urambo, Samwel Sitta lakini kabla ya kwenda mazoezi alfajiri, waliarifiwa kuhusu kifo hicho. “Inasikitisha, lakini ni ya Mungu yote,” alisema Kadutu.
  Jamal Malinzi amesikitishwa na taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Dimani Fumba, Zanzibar, Hafidh Tahir Ali

  Kifo hicho kimemsikitisha Rais Malinzi ambaye alituma salamu za pole na rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai akisema taifa limepata msiba mwingine mzito kwa Mwamuzi wa zamani wa kimataifa wa mpira wa miguu aliyekuwa anatambuliwa/kuwa na beji ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
  Hakika alikuwa kiongozi wa karibu na watu hasa kutokana na michezo ambayo siku zote alikuwa akiota ndoto za kuifikisha mbali hasa ukirejea kuwa ni jana tu Novemba 10, mwaka huu alichaguliwa na wanachama wenzake wa Young Africans  - tawi la Bunge kuwa Katibu wa tawi hilo chini ya Mwenyekiti Venance Mwamoto – Mbunge wa Kilolo mkoani Iringa.
  Ukaribu huo na watu ndio uliompaisha wakati fulani kuwa mmoja watangazaji mahiri wa redio alipoganya kazi hiyo na manguli wengine kama David Wakati kabla ya kuwa Msemaji wa Serikali ya Awamu ya Tano ya SMZ kabla ya kuwa Mbunge wa RahaLeo.
  “Wiki hii imekuwa ngumu kwangu, tumepoteza viongozi wa mfano na wanamichezo mahiri katika kucheza michezo hususani mpira wa miguu na kuuongoza hata kama ni kwa mawazo yao chanya tu. Mheshimiwa Hafidhi ni sehemu ya wanamichezo hao mahiri, ni pigo kubwa hasa kwenye tasnia ya mpira wa miguu. Dua zetu ni Mwenyezi Mungu amghufie na kumrehemu marehemu,” alisema Malinzi.
  Katika salamu zake za rambirambi, Rais Malinzi pia alitoa pole kwa familia ya marehemu Hafidh Tahir Ali, ndugu, jamaa, majirani, na marafiki hususani wapiga kura wa Jimbo la Dimani Fumba kwa kumpoteza kiongozi wao hivyo kuwataka kuwa watulivu wakati huu mugumu kwao.
  Pia Rais Malinzi amesema vifo cha Sheikh Said Mlohammed, Mzee Mheshimiwa Sitta na Mheshimiwa Tahir, vibaki kuwa sehemu ya funzo kwetu katika kujiandaa na maisha ya baadaye kwa sababu zote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea. Inna lillah wainn ilayh  Rajiuun.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MALINZI AHUZUNISHWA NA MSIBA WA HAFIDH ALI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top