• HABARI MPYA

  Saturday, November 12, 2016

  LWANDAMINA AMREJESHA BUSUNGU YANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Yanga, Malimi Busungu ameamua kurejea kwenye timu hiyo baada ya ujio wa kocha mpya, George Lwandamina kutoka Zambia.
  Busungu alikata tamaa kutokana na kutopewa nafasi ya kucheza chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na akasusa tangu Oktoba 1, mwaka huu. 
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo mjini Dar es Salaam, Busungu alisema kwamba amesitisha uamuzi wake wa kuondoka Yanga baada ya mabadiliko ya benchi la Ufundi yanayotaka kufanywa na uongozi.
  Busungu ameamua kurejea Yanga baada ya ujio wa kocha mpya, George Lwandamina kutoka Zambia

  Yanga inataka kuondoa benchi zima la Ufundi Yanga, lililo chini ya Pluijm na wasaidizi wake, wazalendo, Juma Mwambusi na Juma Pondamali kocha wa makipa na kumleta Lwandamina atakayekuwa akisaidiwa na Charles Boniface Mkwasa na Manyika Peter kocha wa makipa.
  Na kwa sababu hiyo, Busungu baada ya kususa tangu asubuhi ya Oktoba 1, siku ambayo Yanga ilimenyana na Simba SC katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kutoka sare ya 1-1 ameamua kurudi kujaribu bahati yake tena.
  “Bado nipo nipo sana Yanga, watu wanasema mimi ninaondoka sijui ninakwenda wapi. Lakini mimi bado nipo nipo sana Yanga. Narudi kwa nguvu zetu kuonyesha uwezo wangu kwa kocha mpya ili anipe nafasi ya kucheza,”alisema.
  Busungu alisema kwamba alikuwa anaumia kuwekwa benchi Yanga wakati kwenye mazoezi alikuwa anafanya vizuri na makocha wanamsifia. “Nikajiuliza mbona wakati Mkwasa yupo (Kocha Msaidizi) Yanga nilikuwa nacheza, inakuwaje sasa hivi kaja Mwambusi sichezi? Nikaona hapa kuna namna, bora niondoke nisije nikaua kipaji changu. Lakini bahati nzuri wamekuja makocha wapya, acha nikomae nijaribu bahati yangu tena,”alisema.
  Busungu alisema kwamba aliumia zaidi baada ya kuondolewa kwenye programu ya mechi dhidi ya Simba SC saa chache kabla ya mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Oktoba 1, mwaka huu.
  “Tulikuwa kambini Pemba wiki nzima. Nilijifua vizuri na makocha wote walinisifia kwamba nilifanya vizuri, ajabu tunafika Dar es Salaam naambiwa Busungu nenda nyumbani, iliniuma sana. Iliniuma kwa sababu nilikuwa nina hamu nao sana Simba na nilijifua ili niwafunge,”alisema.
  Mshambuliaji huyo wa zamani wa Mgambo JKT ya Tanga alisema kwamba tangu hapo hakurudi tena kufanya mazoezi Yanga na alitaka kweli kuondoka kama si taarifa za ujio wa kocha mpya, Lwandamina. “Mimi si mtu wa visingizio, ninarudi Yanga kwa nguvu zangu zote kuonyesha uwezo kwa kocha mpya,”alisema.         
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LWANDAMINA AMREJESHA BUSUNGU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top