• HABARI MPYA

    Tuesday, November 15, 2016

    LWANDAMINA AMLETA JESSE WERE MKALI WA MABAO WA KENYA NA ZESCO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA mpya wa Yanga, George Lwandamina amependekeza wachezaji wawili wasajiliwe dirisha hili dogo, ambao ni kiungo wa ulinzi Mzambia Meshack Chaila na mshambuliaji Mkenya Jesse Were. 
    Chaila na Were wote walikuwa wachezaji tegemeo wa kocha Lwandamina katika kikosi cha Zesco United kilichofika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu kabla ya kutolewa na Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini iliyofanikiwa kutwaa taji hilo.
    Na baada ya Lwandamina kuhamia Yanga, moja ya nafasi ambazo ameona zinahitaji marekebisho ni kiungo cha ulinzi na ushambuliaji na wachezaji sahihi kwa nafasi hizo kati ya wote aliokuwa anafanya nao kazi Zesco ameona ni Chaula na Were.
    Mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Jesse Were anatarajiwa kuja Yanga akitokea Zesco United ya Zambia 

    BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE inaamini Yanga imekwishafikia makubaliano na wachezaji hao wote wawili na wakati wowote kuanzia leo watawasili nchini kwa ajili yab kusaini.
    Lakini Yanga italazimika kukata wachezaji wawili wa kigeni ili kuwasajili Chaila na Were kwa sababu tayari imekwishatimiza idadi ya wachezaji saba wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu.
    Wachezaji wa kigeni wa Yanga kwa sasa ni mabeki Mbuyu Twite kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Vincent Bossou kutoka Togo, viungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda, Thabani Kamusoko, washambuliaji Donald Ngoma kutoka Zimbabwe, Obrey Chirwa kutoka Zambia na Amissi Tambwe kutoka Burundi.
    Bado haijajulikana Lwandamina atawaondoa akina nani kati ya Twite, Bossou, Niyonzima, Kamusoko, Ngoma, Chirwa na Tambwe iwapo atafanikiwa kuwasajili Chaila na Were.
    Lakini kwa mtazamo wa haraka wanaoweza kuondoka ni Twite ambaye inadaiwa amekwishaomba kustaafu na Chirwa ambaye licha ya kusajiliwa Agosti tu mwaka huu, lakini hajaweza kuwapiku washambuliaji aliowakuta Ngoma na Tambwe.
    Lwandamina anatarajiwa kuchukua nafasi ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyeongoza Yanga SC kwa awamu mbili tangu mwaka 2014. 
    Inadaiwa wasaidizi wa Pluijm, Juma Mwambusi (Kocha Msaidizi), kocha wa makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Mtunza Vifaa vya timu, Mahmoud Omar ‘Mpogolo’ na Dk Edward Bavu pia wataondoka na 
    Lwandamina atasaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.  
    Pluijm anaondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 128, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23.  Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014 baada ya kumrithi Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts, Pluijm alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana alipomrithi Mbrazil Marcio Maximo, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.
    Na anaondoka baada ya msimu mzuri uliopita, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
    Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria. Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
    Na kwa mafanikio hayo, haikuwa ajabu Pluijm akishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu uliopita. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LWANDAMINA AMLETA JESSE WERE MKALI WA MABAO WA KENYA NA ZESCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top