• HABARI MPYA

  Tuesday, November 08, 2016

  KICHUYA: SIMBA TUTAZINDUKA MBELE YA PRISONS KESHO MBEYA

  Na David Nyembe, MBEYA
  NYOTA wa Simba SC, Shizza Ramadhani Kichuya amesema kwamba anaamini watazinduka katika mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Simba SC watakuwa wageni wa Prisons kesho Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya katika mfululizo wa Ligi Kuu wakitoka kufungwa 1-0 na African Lyon Jumapili Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Na Kichuya, kinara wa Ligi Kuu hadi sasa akiwa amefunga mara 10 amesema; “Tuliteleza katika mchezo uliopita na sasa tunaelekeza nguvu zetu katika mchezo ujao, kwa matumaini makubwa ya kushinda,”.
  Shizza Kichuya akiwa mwenye masikitiko baada ya mchezo na African Lyon
  Kichuya hakuamini kabisa kilichotokea juzi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam
  Kichuya amesema makosa ambayo yalijitokeza katika mchezo uliopita benchi ka Ufundi limekwishayafanyia kazi na wanatarajia kesho mambo yatakuwa mazuri. 
  Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog na Msaidizi wake Mganda Jackson Mayanja walikuwa wana kikao na wachezaji juzi Dar es Salaam kabla ya safari ya Mbeya jana kujadili matokeo ya African Lyon na mchezo wa kesho.
  Na kwa kiasi kikubwa kipigo hicho ambacho hakikutarajiwa kimemuumiza kila mmoja ndani ya Simba na wachezaji kwa ujumla wamedhamiria kushinda kesho ili kurudi katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la kwanza la ubingwa wa Ligi Kuu tangu mwaka 2012.
  Kipigo hicho kilichotokana na bao pekee la Abdallah Mguhi ‘Messi’ kinaifanya Simba ibaki na pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 14 ingawa, inaendelea kuongoza Ligi Kuu mbele ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 30 za mechi 14 pia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KICHUYA: SIMBA TUTAZINDUKA MBELE YA PRISONS KESHO MBEYA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top